Anna Ruhasha, Geita
Mbunge Geita Mjini, Constantine Kanyasu amewataka wananchi kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Geita kufika katika maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye sekta ya madini ili kupata elimu itakayowasaidia kubadilisha mfumo wa maisha yao hasa kufanyabiashara itakayowaongezea kipato.
Kanyasu ameyasema hayo Ijumaa Septemba 17, alipofika katika maonesho hayo na kutembelea mabanda mbali mbali yaliyopo katika maonesho hayo kwa malengo ya kutoa elimu kwa wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika maonyesho hayo ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji, Kanyasu amesema kwa miaka minne mfululizo maonesho yanayofanyika mkoani humo yameleta heshima na kuwahimiza wananchi kuyatumia kwa faida ikiwamo kujielimisha.
“Haya ni maonesho ambayo yanatupa heshima sisi wananchi wa Geita na Mji wa Geita sababu sasa yameandaliwa hapa mwaka wa Nne sasa, lakini yameshirikisha vyombo na tasisi muhimu katika maendeleo ya nchi. Ukiangalia hapa leo mtu anayetaka kufanyabishara anapata elimu, anayetaka kupata huduma kutoka kwenye taasisi yoyote anapata na kwa wakati.
“Hivyo tuendelea kuyatumia maonyesho haya ambayo yamekuwa yakiimarika kila mwaka na kuchukua sura ya mikataifa na kuhamasisha washiriki wa nje ya nchi,” amesema Kanyasu.
Aidha, ametumia nafasi hiyo pia kuipongeza serikali ya mkoa pamoja na Wizara ya adini kushiriki kikamilifu kwa kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa kivutio cha kuelimisha jamii kwa masula mbali mbali ya kimaendeleo.
“Maonesho haya siyo ya kuonyeshana wao wenye mabanda bali ni kukutanisha wadau mbalimbali kutoka kwenye nyanja tofautitofauti,” amesema Kanyasu.
Wakati huohuo, Kanyasu ameupongeza mgodi wa Geita Gold Mine(GGM) kwa kuendelea kuwa wadhami wa maonesho hayo kwa kipindi chote ambapo amesema yeye kama mbunge wa Geita Mjini anafahamu vizuri mchango wa mgodi huo kwenye jamii.
Maonesho hayo yamebeba kauli mbiu ya “Sekta ya madini kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu”.