KAMPUNI ya Liberty Media ya Marekani, imethibitisha kununua mashindano ya mbio za Formula 1 kwa dola za Marekani bilioni nne.
Uamuzi wa kampuni hiyo umedaiwa kuvunja minong’ono ya mwaka mmoja uliopita kuhusu mmiliki halali wa mbio hizo.
Hata hivyo, Bernie Ecclestone, atabaki kuwa Mkurugenzi Mkuu wa mashindano hayo lakini Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya 21 Century Fox, Chase Carey, atakuwa Mwenyekiti mpya wa kampuni hiyo.
Kampuni ya Liberty Media inadaiwa kuwekeza katika michezo na burudani mbalimbali duniani.
Kampuni hiyo inayomilikiwa na bilionea, John Malone, pia ina mpango wa kununua hisa kutoka kwa kampuni nyingine ambazo zinamiliki mashindano makubwa ya mbio za magari duniani.
Kampuni hiyo ilinunua mashindano hayo kwa jumla ya bilioni nane kwa kujumuishwa bilioni nne za Marekani ambazo zilitolewa kwa kulipa deni la mashindano hayo.
Liberty Media ilinunua hisa kutoka kampuni binafsi ya CVC Capital ambayo ilikuwa ikizimiliki tangu 2012.
Lakini kampuni hiyo imekuwa ikikosolewa kwa kuchukua faida kubwa katika michezo, ambayo imekuwa na mdororo wa haki ya matangazo miaka ya hivi karibuni.
Mhariri wa uchambuzi wa michezo wa Kampuni ya BBC Sport, Dan Roan, alisema kwamba ununuzi huo ni wa kihistoria katika michezo ambao ulikuwa muhimu kufanyika kwa ajili ya mashindano hayo.