Veronica Simba, Manyara
Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani, amesema wananchi hawapaswi kulipia nguzo wanapotaka kuunganishiwa umeme kwani hilo ni jukumu la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Akizungumza na wananchi katika Wilaya za Babati na Mbulu mkoani Manyara jana Julai 28, Waziri Kalemani pia ametoa onyo kwa mtumishi yeyote wa Tanesco atakayebainika kutomuunganishia umeme mteja aliyelipia huduma hiyo kwa kisingizio cha kutokuwepo nguzo au kumtaka alipie.
“Wananchi nchi nzima muelewe, hampaswi kulipia nguzo na kwamba atakayebainika kwenda kinyume na maagizo hayo ya serikali, atachukuliwa hatua za kinidhamu mara moja,” amesema.
Katika hatua nyingine Dk. Kalemani alitoa wito kwa wananchi vijijini, katika maeneo ambayo tayari miundombinu ya umeme imefika, kulipia Sh 27,000 tu ili waunganishiwe huduma hiyo.