Na ELUD NGONDO, KYELA
WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ametoa siku 28 kwa Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kukamilisha ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa zaidi ya kilometa 20 na kuwashwa kwenye makazi ya wananchi katika kata mbili wilayani Kyela.
Waziri Kalemani, alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi kataka Kata ya Ipande ambako alistushwa baada ya kuelezwa na wananchi kuwa kata za Nkokwa na Ipande hazijawahi kufikiwa na umeme hata kwenye kijiji kimoja tangu Serikali ilipoanza mpango wa kusambaza umeme vijijini.
Alisema haiwezekani kata nzima za Ipande na Nkokwa ziwe hazijafikiriwa na umeme kwa kipindi chote tangu Serikali ilipoanza kupeleka umeme katika vijiji vyote na kitendo hicho kinaonyesha kuna mahali uzembe unafanyika miongoni mwa watekelezaji wa mpango huo.
Aliiagiza wakala huo kwa kushirikiana na Tanesco kuanza mara moja kazi ya kuchimbia nguzo kuelekea kwenye kata hiyo na kutoa mwezi mmoja kazi hiyo ikamilike na umeme uwashwe kwenye makazi ya wananchi.
“Naagiza kazi ianze kufikia 28, Aprili, mwaka huu umeme uwashwe kwenye kata hizi za Nkokwa na Ipande, ikiwa agizo hili halitatekelezwa nawambieni watendaji wangu wa Rea na Tanesco mtapungua au kumalizika kabisa kwenye nafasi zenu,” alisema Dk. Kalemani.
Alisema suala la usambazaji wa umeme vijijini sio la hiyari bali ni la lazima kutokana na Serikali kuazimia vijiji vyote nchini vifikiwe na umeme na kila mwananchi apewe fursa ya kuingiza umeme kwenye nyumba yake.
Hata hivyo Wakati Dk. Kalemani akitoa agizo hilo, Mbunge wa Kyela ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hurrison Mwakyembe akainuka na kumweleza kuwa siku hiyo ya April 28, mwaka huu kutakuwa na tukio kubwa la kitaifa hivyo akamuomba awaongeze watendaji wake japo siku tatu mbele.
“Mheshimiwa Waziri, 28 Aprili timu yetu ya Vijana wenye Umri wa Chini ya Miaka 17, Serengeti Boys watakuwa uwanjani wakiwania taji la Afrika, hivyo naamini watanzania wote watakuwa wakifuatilia mchezo huo, nakuomba usogeze mbele japo kwa siku tatu ili na hawa watendaji nao wapate fursa ya kuiangalia timu yetu ikiwa uwanjani,” alisema Dk. Mwakyembe.
Baada ya ombi hilo, Dk. Kalemani ambaye alikubali kusogeza Mbele hadi 2 Mai, Mwaka huu aliahidi kurejea tena wilayani Kyela kwenda kukagua utekelezaji wa mradi huo.
Akizungumza na wananchi wa Ipinda, Waziri Dk. Kalemani alipiga marufuku tabia ya Shirika la Umeme kupandisha bei ya kuunganishia wananchi umeme majumbani baada ya kukabidhiwa miradi ya Rea vijijini.
Alisema amegundua Tanesco wakishakabidhiwa miradi hiyo, hupandisha bei ya kuunganishia umeme majumbani kutoka Sh 27,000 hadi 177,000 jambo ambalo alidai ni kinyume na maagizo ya Serikali.