30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge wa CCM ajitolea kuwasomesha wasichana

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MBUNGE wa Viti Maalumu, Mariamu Ditopile (CCM), amesema atawalipia ada wanafunzi wote wa kike watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mkoani Dodoma.

Ditopile alitoa kauli hiyo mjini Dodoma mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema ameamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuguswa na jitihada zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli katika sekta ya elimu.

“Kwa hiyo, nimeamua kuwalipia ada wanafunzi wote wa Mkoa wa Dodoma ambao watakuwa wamefaulu  na kujiunga na kidato cha tano.

“Mimi kama mbunge, nimeguswa na jitihada hizi za Serikali yetu chini ya rais na mimi leo hii nimelazimika kutoa mchango kwa watoto wetu ili nionekane niko pamoja na Serikali yetu,” alisema Ditopile.

“Pamoja na hayo, huko tunakokwenda, tutazindua programu maalumu ya kuwawezesha wasichana ambao wamefaulu kidato cha nne kwenda kidato cha tano watakaochaguliwa kujiunga kidato cha tano, tuweze kuwafadhili ili waweze kupata elimu.

“Hilo jambo litaratibiwa na ofisi ya vijana wa UVCCM, Mkoa wa Dodoma pamoja kwa kushirikiana na ofisi ya elimu ya mkoa kupitia maofisa elimu wa wilaya.

“Tutakapowatambua ni wangapi wamefaulu na wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano, mabinti hao tutawapa ufadhili na gharama zitalipwa na mimi mbunge kupitia vijana wa Mkoa wa Dodoma,” alisema Ditopile.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa wa Dodoma, Bill Chidabwa, alisema wataanza ziara Aprili 29, mwaka huu ya kukagua miradi ya kimkakati ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa stendi ya mabasi jijini Dodoma pamoja na ujenzi wa soko la kisasa.

Mwisho.

Katibu Mkuu Tamisemi awakumbusha wakurugenzi

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

KATIBU Mkuu Tamisemi, Joseph Nyamhanga, amewataka wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha hoja zote zilizoibuliwa kwenye taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zinajibiwa na kuyafanyia kazi mapendekezo ya wakaguzi kwa kuanzia na wakaguzi wa ndani.

Nyamhanga alitoa kauli hiyo jana jijini hapa wakati akizungumza  kwenye kikao kazi cha upokeaji na uhakiki wa taarifa za majibu na mipango kazi ya utekelezaji wa hoja na mapendekezo ya CAG kwa hesabu za mamlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2017/18 .

Alisema kwamba, ni muhimu hoja zote zifanyiwe kazi haraka na kwa ufasaha ili kunusuru upotevu wa fedha na kuboresha utendaji na kuimarisha utawala bora, jambo ambalo ndio msingi wa ukaguzi.

“Tukifanya hivyo, hoja zisizo za lazima zitaondoka na hata wakaguzi hawatatumia muda mwingi katika kufuatilia mambo ya msingi zaidi katika kuboresha utendaji.

“Katika kujibu hoja za CAG na kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa maagizo ya CAG ya hesabu za mwaka 2016/17, imeonekana kufikia Januari 2019, jumla ya hoja asilimia 47 zilifungwa na asilimia 53 zilikuwa bado hazijajibiwa,” alisema Nyamhanga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi na Ufuatiliaji wa Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa, Miriam Mmbaga, alisema lengo la kikao hicho lilikuwa ni kuwawezesha watendaji hao kujibu hoja za CAG na kuongeza uwajibikaji katika utendaji wao wa kazi ili hoja hizo zisijitokeze tena katika halmashauri zao.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, alisema kwa niaba ya wakurugenzi wa halmashauri, halmashauri zimekuwa zikikabiliana na changamoto mbalimbali katika kujibu hoja za ukaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles