Na Lilian Justice, Morogoro
SERIKALI imesema haitawafumbia macho maofisa utumishi wazembe watakaoshindwa kusimamia idara zao.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alipozungumza katika kikao kilichokutanisha watumishi wa umma kutoka idara mbalimbali za Serikali.
Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wake wanapatiwa huduma stahiki pindi wanapofika katika ofisi mbalimbali na hivyo haitakubali maofisa utumishi waliopewa madaraka kuona wanashindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu katika sehemu za kazi.
“Lengo kuu la kufanya kikao hicho ni kuwakutanisha watumishi wa umma kutoka idara mbalimbali ili kufanya majadiliano na kutiana ari,” alisema Kairuki.
Aliwataka watumishi hao kuhakikisha wanajiwekea utararibu wa kukusanya kero mbalimbali za watumishi walioko chini yao ili Serikali iweze kuzishughulikia kwa haraka.