27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Wasichana wafunika kidato cha sita

2

*Wavulana nao wawaburuza masomo ya sayansi

*Hisabati bado jipu, Azania yaangukia pua, 25 wafutiwa matokeo

*Tabora Boys, Mzumbe, Ilboru, Kibaha zachomoza kumi bora

 

Na Veronica Romwald

BARAZA la Mitihani nchini (NECTA) limetangaza matokeo ya kidato cha sita (ACSEE) ambayo pamoja na mambo mengine yanaonesha wasichana wanaongoza kwa ufaulu wa asilimia 98.59 dhidi ya wavulana ambao wamefaulu kwa kiwango cha asilimia 97.55.

Matokeo hayo yanaonesha kuwa kati ya wasichana 27,717 walioandikishwa kufanya mtihani huo 26,977 wamefaulu na waliofeli wakiwa 740.

Kwa upande wa wavulana kati ya 47,179 walioandikishwa kufanya mtihani huo waliofeli ni 2,605 wakati waliofaulu wakiwa 44,574.

Licha ya matokeo hayo kuonesha wasichana wengi wamefaulu, hata hivyo wavulana ndio wanaongoza katika ufaulu wa somo la sayansi kwa kushika nafasi nane kati ya kumi bora huku wasichana wakiwa wawili pekee.

Matokeo hayo yalitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Charles Msonde, katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa matokeo hayo ambayo yamechakatwa kwa kutumia mfumo wa ‘division’, baadhi ya shule kongwe za Serikali ambazo katika miaka ya hivi karibuni zilionekana kufanya vibaya na hivyo kufuta rekodi nzuri ilizoziweka miaka ya nyuma, zimeonekana kurudi katika chati ya kumi bora ikiwamo Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, Kibaha, Mzumbe na Ilboru.

Shule ya wavulana Tabora imeongoza kwa kutoa mwanafunzi wa kwanza bora katika somo la sayansi ambaye ni Hassan Gwaay, aliyekuwa akichukua mchepuo wa PCM.

Shule ya Sekondari Tandahimba ya mkoani Mtwara nayo imeonekana kuchomoza katika orodha ya shule kumi bora kitaifa ikitanguliwa na Kisimiri ambayo imeshika nafasi ya kwanza, Feza Boys (2), Alliance Girls (3), Feza Girls (4), Tabora Boys (5),  Marian Boys (6), Kibaha (7), Mzumbe (8)  na Ilboru (9).

Lakini wakati shule hizo ziking’ara, shule kongwe ya Serikali ya Azania iliyoko Dar es Salaam imeanguka vibaya katika matokeo hayo kwa kushika nafasi ya tisa kati ya kumi kwenye orodha ya shule zilizofanya vibaya.

Katika orodha hiyo, shule saba za sekondari zilizoko Unguja visiwani Zanzibar ambazo ni Mpendae, Ben Bella, Tumekuja, Jang’ombe, Kiembesamaki, Al-Ihsan Girl’s na Lumumba nazo zimefanya vibaya pamoja na Green Bird Boys ya Kilimanjaro.

Matokeo hayo pia yanaonesha kuwa somo la hisabati bado ufaulu wake umeendelea kuwa chini likiwa limeshika nafasi ya 12 kati ya masomo 13 yaliyofanywa.

Akitangaza matokeo hayo, Dk. Msonde alisema ufaulu wa jumla katika mtihani huo umeonesha kushuka kidogo kwa kiwango cha asilimia 0.93, kutoka asilimia 98.87 mwaka jana hadi 97.94 mwaka huu.

“Ukilinganisha na mwaka jana, takwimu za ufaulu kimasomo zinaonesha kushuka kwa ufaulu. Katika somo la sayansi kati ya asilimia 5.36 na 8.9, sanaa kati ya asilimia 0.00 na 4.43 na somo la biashara kati ya asilimia 1.7 na 6.9,” alisema.

Alisema somo la historia limeshika nafasi ya kwanza kwa ufaulu wa asilimia 99.96, Kiswahili 99.94, Jiografia 98.96, Economics 98.00, Commerce 97.26, Agricultural Science 96.41, Kiingereza 95.50, biolojia 93.41, Accountancy 92.91, Kemia 87.50, Fizikia 80.34 Hisabati 76.35 na General Studies 71.24.

Alisema hata hivyo ubora wa ufaulu unazidi kuimarika kwa kuwa idadi ya watahiniwa waliofaulu vizuri katika daraja la 1, 11 na 111 imeongezeka kwa asilimia 3.72 kutoka asilimia 89.41 mwaka jana hadi asilimia 93.13 mwaka huu.

Alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja unaonesha jumla ya watahiniwa 60,407 sawa na asilimia 93.13 wamefaulu katika daraja 1, 11 na 111 ambapo wasichana ni 23,045 sawa na asilimia 94.43 na wavulana 37,362 sawa na asilimia 92.35.

“Jumla ya watahiniwa 74,896 waliandikishwa kufanya mtihani huo, wasichana wakiwa 27,717 sawa na asilimia 37.01 na wavulana ni 47,179 sawa na asilimia 62.99. Kati ya watahiniwa waliosajiliwa 65,585 walikuwa wa shule na 9,311 walikuwa wa kujitegemea,” alisema.

Alisema kati ya watahiniwa 74,896 waliokuwa wamesajiliwa, watahiniwa 73,940 sawa na asilimia 98.72 walifanya mtihani huo huku 956 sawa na asilimia 1.28 hawakufanya kutokana na sababu mbalimbali.

“Kati ya watahiniwa wa shule 65,585 waliosajiliwa, 65,276 sawa na asilimia 99.53 walifanya mtihani huo, wasichana wakiwa 24,467 sawa na asilimia 99.69 na wavulana 40,809 sawa na asilimia 99.43 na watahiniwa 309 sawa na asilimia 0.47 hawakufanya mtihani,” alisema.

Dk. Msonde alisema kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea kati ya 9,311 waliosajiliwa, 8,664 sawa na asilimia 93.05 ndio waliofanya mtihani na kwamba 647 sawa na asilimia 6.95 hawakufanya.

“Jumla ya watahiniwa 71,551 sawa na asilimia 97.32 ya waliofanya mtihani, wasichana waliofaulu ni 26,977 sawa na asilimia 98.31 na wavulana ni 44,574 sawa na asilimia 96.73. Mwaka jana waliofaulu walikuwa ni 38,853 sawa na asilimia 97.65,” alisema.

Alisema watahiniwa wa shule 63,528 sawa na asilimia 97.94 ya waliofaulu wasichana ni 24,062 sawa na asilimia 98.59 na wavulana ni 39,466 sawa na asilimia 97.55.

Alisema kati ya watahiniwa wa kujitegemea 8,664 walioandikishwa  kufanya mtihani huo, 8,023 sawa na asilimia 92.64 walifaulu na kwamba mwaka jana waliofaulu walikuwa 4,076 sawa na asilimia 88.34.

Alisema ubora wa shule umepangwa kwa kutumia kigezo cha wastani wa pointi (GPA) ambapo A ni 1, B-2, C-3, D-4, E-5, S-6 na F-7.

Pamoja na hilo, Dk Msonde alisema Baraza la Mitihani pia limewafutia matokeo watahiniwa 25 waliobainika kufanya udanganyifu.

“21 kati yao waliofutiwa matokeo ni wa shule na wanne wa kujitegemea. Pia tumetoa fursa ya kurudia kufanya mitihani yote kwa watahiniwa 36 na baadhi ya mitihani kwa watahiniwa 10 ambao walishindwa kufanya na wenzao kutokana na matatizo ya kiafya,” alisema.

Wakati huo huo: Baraza limetangaza matokeo ya mtihani wa Ualimu Daraja A (GATCE) na mtihani wa stashahada ya ualimu wa sekondari (DSEE).

Dk. Msonde alisema katika mtihani wa GATCE jumla ya watahiniwa 10,747 sawa na asilimia 99.81 wamefaulu, wasichana wakiwa 5,065 sawa na asilimia 99.88 na wavulana 5,682 sawa na asilimia 99.75.

Alisema katika mtihani wa DSEE watahiniwa 337 sawa na asilimia 84.46 ya waliofanya mtihani huo wamefaulu ambapo wasichana ni 72 sawa na asilimia 74.23 na wavulana ni 265 sawa na asilimia 87.75.

“Watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani wa GATCE walikuwa 10,944, wasichana 5,103 sawa na asilimia 46.63 na wavulana 5,841 sawa na asilimia 53.37. Kati yao 10,887 sawa na asilimia 99.48 ndio waliofanya mtihani wasichana wakiwa 5,089 sawa na asilimia 99.73 na wavulana 5,798 sawa na asilimia 99.26,” alisema.

Alisema watahiniwa 57 sawa na asilimia 0.5 hawakufanya mtihani huo wasichana wakiwa 14 sawa na asilimia 0. 27 na wavulana ni 43 sawa na asilimia 0.74.

Katibu Mtendaji huyo alisema katika mtihani wa DSEE, watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 418, wasichana ni 98 sawa na asilimia 23.44 na wavulana 320 sawa na asilimia 76.56.

“Kati ya watahiniwa hao waliosajiliwa 415 walifanya mtihani ambapo wasichana ni 97 sawa na asilimia 98.98 na wavulana ni 318 sawa na asilimia 99.38, watahiniwa watatu sawa na asilimia 0.72 akiwemo msichana mmoja sawa na asilimia 1.02 na wavulana wawili sawa na asilimia 0.63 hawakufanya mtihani,” alisema.

Alisema baraza limefuta matokeo ya mtahiniwa mmoja ambaye alibainika kufanya udanganyifu katika mtihani wa GATCE.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles