Mgomo wavuruga masomo Uingereza

DARASANI

LONDON, UINGEREZA

MAELFU ya wanafunzi nchini Uingereza wamejikuta wakikosa masomo baada ya Muungano wa Taifa wa Walimu (NUT) kuendesha mgomo wa siku moja kupinga punguzo la bajeti katika sekta hiyo.

Takwimu zilionesha shule mbili kati ya tatu zilibakia wazi licha ya kuwapo kwa mgomo huo ambao walimu mbali ya kupinga kupunguzwa kwa malipo wanalalamikia wingi wa kazi.

Waziri wa Elimu, Nicky Morgan, alisema mgomo huo haukuwa na msingi na ni haribifu.

Maofisa wa NUT waliungana na walimu kote England kufanya mgomo huo wa saa 24 huku mamia ya shule yakiathirika, iwe kwa kufungwa kabisa au masomo kuzorota.

“Tumeshuhudia kupunguzwa kwa kiwango cha fedha kwa asilimia 10 kipindi cha mwaka mmoja, ni kitu kinachoathiri maisha yetu na ari ya kazi,” alisema mwalimu mmoja katika shule ya sekondari mashariki mwa London.

Alisema wanachopinga ni kupunguzwa kwa kiwango kikubwa cha bajeti wakati huo huo kazi zikiwa zimeongezeka huku baadhi ya walimu wakiachishwa kazi ili kubana matumizi.

“Kila mwisho mwa wiki na nyakati za jioni tunatakiwa kuwapo shule. Nadhani ni kitu kibaya kwetu na kwa watoto ambao wanaishia kuchoka,” alisema mwalimu mwengine.

Kaimu Kiongozi wa NUT, Kevin Courtney, alisema bajeti za shule haziendani na kupanda kwa gharama ya maisha na ameitupia lawama serikali kwa kutokuwa tayari kwa majadiliano.

“Kinachotokea sasa ni kwa sababu serikali hairuhusu bajeti kuendana na mfumuko wa bei na tulikuwa tayari kwa majadiliano lakini waziri wa elimu hauoni ukweli huo,” alisema.

Lakini Waziri Morgan ameukosoa mgomo huo akisema unawaathiri wanafunzi na kuwaletea usumbufu wazazi na kuharibu sifa ya taaluma hiyo machoni mwa umma.

Alisema serikali imelinda bajeti ya shule huku maeneo mengine ya matumizi yasiyo na lazima yakipunguzwa.

“Matumizi katika elimu ni makubwa na mwaka huu yameshuhudia  pauni bilioni 40. Yamepanda wa pauni bilioni nne tangu mwaka  2011-12,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here