Na ELIZABETH HOMBO -DAR ES SALAAM
IKIWA ni zaidi ya mwezi mmoja tangu timu ya Barrick ilipowasili nchini kufanya mazungumzo na Tanzania, Rais Dk. John Magufuli, amefichua sababu za kutowekwa wazi kwa wajumbe wa Tanzania, huku akisema wale wa Barick wameongezeka kutoka 14 hadi 25.
Akizungumza baada ya kupokea ripoti mbili za Bunge, ikiwamo ya Tanzanite na Almasi, Rais Magufuli aligusia taarifa ya hivi karibuni ya Acacia ya kupunguza shughuli kwenye mgodi wa Bulyanhulu, mpango utakaoandamana na kupunguza wafanyakazi.
Sababu ya usiri timu ya Tanzania
Rais Magufuli alisema wapo Watanzania ambao ni wazalendo sana na ndio maana hawa wazungu wa dhahabu bado wapo wanazungumza, walikuja 14 mpaka leo wako 25, wanaendelea kuja tu, wanajaribu waongeze, sisi idadi yetu ni ile ile.
“Lakini tumemamua kuwa-protect (kuwalinda), wapo watu waliosema mbona hatuwaoni, tukiwa-expose (tukiwaweka hadharani) maana yake tunawaleta katika maisha ya ajabu. Lakini muamini wapo Watanzania waaminifu ambao wanazungumza na hao (Barrick), nataka Watanzania tuvumilie hii ni kazi nzito,”alisema Magufuli.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu siku moja baada ya timu hizo kuanza majadiliano, ilisema kuwa timu ya Tanzania inaongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi huku ile ya Barrick ikiongozwa na Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa kampuni hiyo, Richard Williams.
Acacia
Akizungumzia taarifa ya Acacia, Rais Magufuli alisema wawekezaji hao wakiondoka, anaweza hata kuwaambia wananchi wa kawaida wakachimbe, tatizo ni kuwa tu watafariki wengi.
“Nasikia wengine eti wanatishia kupunguza wafanyakazi mimi nilitamani waseme wangeondoka, kwa sababu wakiondoka tutachukua wananchi wa kawaida wakachimbe kule, tatizo itakuwa tu ku-control maisha yao tu.
“Kama wamefukuza watu 2,000 tukiruhusu wananchi wa jirani pale Nyamongo wakachimbe mle tutatengeneza ajira milioni moja na of course vifo vitakwepo… Wako watu wataacha kazi wataenda mle… Mle sasa ndio itakuwa kazi, tumepewa hizi rasilimali ni zetu, wasijaribu kututisha wao ndio wataendelea kutishika,”alisema Rais Magufuli.
Alisema inawezekana Tanzania inahudumia nchi zingine kutokana na namna wawekezaji wanavyonya rasilimali zake.
“Umasikini wetu na bajeti yetu hii, inawezekana tunahudumia nchi nyingine, ninyi mnatengeneza bajeti ya Sh bilioni 30 wakati wao wanachukua Sh bilioni 600 au Sh trilioni 600 halafu wanakwenda kutengeneza bajeti yao wanakuja na vi-complimentary vyao mnasema hawa wafadhili, sisi ndio wafadhili,”alisema.
Sehemu ya taarifa iliyotolewa na Acacia mwanzoni mwa wiki hii ilisema. “Acacia imeamua kuanza mpango wa kupunguza operesheni na matumizi pale Bulyanhulu ili kuboresha ustahimilivu wa biashara yetu.
“Mpango huu utahusisha utunzaji wa mali zote zisizohamishika na mitambo, ili kuwezesha mgodi kurejea katika utendaji wa kawaida, pale zuio litakapo ondolewa na mazingira ya uendeshaji biashara kutulia.
“Baada ya tangazo hili, Bulyanhulu itaanza mashauriano na wadau wake kama sehemu ya mpango wa kupunguza shughuli za kioperesheni.
“Kama sehemu ya utekelezaji wa mpango huu, shughuli za chini ya ardhi zitasitishwa na uchenjuaji wa miamba unapangiwa kusitishwa ndani ya wiki nne,” alisema.
Taarifa hiyo ilisema kuchukuliwa kwa hatua hizo, kutafanya baadhi ya wafanyakazi 1,200 wa kampuni hiyo kupunguzwa na wakandarasi 800 waliopo, baadhi yao pia watakosa ajira.
“Tangu zuio la usafirishwaji wa makinikia nje ya nchi ilipowekwa Machi 3, na kuathiri asilimia 35 ya uzalishaji wa kampuni hiyo kwa mwaka huu, Acacia imekuwa na ongezeko la hifadhi ya makinikia yenye thamani ya dola za Marekani milioni 265 nchini.