Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli, amefanya mazunguzo kwa simu na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ambaye amemuhakikishia kuwa nchi yake ipo tayari kukuza uhusiano wake na Tanzania hususan kusaidia juhudi za kuimarisha uchumi.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilieleza Merkel alimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwamo kupambana na rushwa na kuimarisha miundombinu.
Kutokana na mafanikio hayo Kansela Merkel, alisema Ujerumani itawaleta wafanyabiashara watakaowekeza katika maeneo mbalimbali ya kuimarisha uchumi ikiwamo kujenga kiwanda cha mbolea ambacho kitakuwa kikubwa kuliko vyote Barani Afrika.
Alisema Ujerumani imedhamiria kuunga mkono juhudi za ujenzi wa viwanda Tanzania na kwamba ana matumaini kuwa kiwanda kikubwa cha mbolea kitakachojengwa nchini kitasaidia kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha kilimo kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Pamoja na hali hiyo alitoa wito wa kuimarishwa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Permanent Comission – JPC) na amemwalika kwa mara ya pili, Rais Magufuli kutembelea Ujerumani, ziara ambayo itatanguliwa na ziara ya mawaziri wa Tanzania kukutana na mawaziri wa Ujerumani.
Kwa upande wake, Rais Magufuli alimshukuru Kansela Merkel kwa kumpigia simu na kueleza dhamira yake ya kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Ujerumani.
Amebainisha Tanzania itahakikisha inajenga mazingira mazuri katika maeneo yote ya ushirikiano yakiwamo yabiashara na uwekezaji.
Rais Magufuli alimpongeza Kansela Merkel kwa uongozi wake wa zaidi ya miaka 13 akiwa Kansela wa Ujerumani na alimhakikishia Tanzania itadumisha na kukuza zaidi ushirikiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alikuwa na mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman J.A. Al Thani, Ikulu Dar es Salaam.
Viongozi hao walizungumzia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Qatar na dhamira yao ya kuhakikisha uhusiano na ushirikiano huo unaendelezwa na kukuzwa zaidi hususan katika masuala ya uwekezaji katika gesi, madini, utalii na miundombinu ya barabara, bandari, nishati, reli na huduma za kijamii.
Rais Magufuli alimshukuru Sheikh Mohammed kwa kuja nchini pamoja ujumbe wa wawekezaji wenye dhamira ya kuwekeza Tanzania.
Amemuomba ampelekee salamu za shukrani kwa Mtawala wa Taifa la Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani kwa kuendeleza uhusiano na Tanzania.