33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

JPM amtumbua OCD Njombe, amrejesha papo hapo

NORA DAMIAN Na ELIZABETH KILINDI-DAR/NJOMBE

RAIS Dk. John Magufuli amemtumbua Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Njombe (OCD), SSP Sifaeli Pyuza, kisha kumsamehe papohapo kutokana na kukerwa na mauaji ya watoto saba yaliyotokea wilayani humo.

Watoto hao waliuawa mwanzoni mwa mwaka huu huku chanzo cha mauaji hayo kikitajwa kuwa ni imani za kishirikiana.

Akizungumza jana wakati wa ziara yake mkoani Njombe, Rais Magufuli alisema mkoa huo umefanya vizuri katika mambo mengi lakini mauaji ya watoto yameutia doa.

“Suala hili halikutakiwa kuchukua muda mrefu, ndio maana RPC (aliyekuwepo awali) nimemtoa kwa sababu alishindwa kusimamia hii kazi, ninataka mambo yatendeke haraka.

“Anapotea mtoto wa kwanza mpaka wanafikia saba wewe RPC mbona wako hawajapotea, haiwezekani tunaleta polisi wa operesheni kutoka Dar es Salaam kuja kusimamia wakati hapa kuna polisi.

“OCD wa hapa bado yupo, naye aondoke, najua yuko hapa ananilinda naye si OCD hapa. Ni lazima watu tufike mahali tuwe tunawajibika katika maeneo yetu, watoto saba wanapotea huchukui hatua upo na nyota zako lazima uwajibike kwa matendo yako,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alitahadharisha kuwa kama mauaji hayo yakijirudia safu nzima ya uongozi wa mkoa itaondoka.

“Siku nyingine ikitokea namna hiyo Mkuu wa Mkoa, DC (Mkuu wa Wilaya), DAS (Katibu Tawala), katibu tarafa mpaka mwenyekiti wa kijiji…ikiwezekana na katibu wa CCM wote wanaondoka ili tufike mahali tuwe tunachukua hatua haraka.

“Huwezi ukatajirika kwa kuua mtoto, saa nyingine unaua mtoto wako ni mambo ya ajabu sana, mimi sijatia sahihi mtu kunyongwa lakini nikiletewa kesi kama hizi nitamuomba malaika wangu inawezekana nikasaini.

“Haiwezekani tukaendekeza mambo ya kishirikina kwamba ukimuua mtoto ndipo utapata mahindi mengi ni ujinga. Watoto badala ya kwenda shuleni wakiwa wana raha wakiwa wana raha wanacheza mpaka wanasindikizwa na mama zao mtalima saa ngapi, ni mateso ni lazima tabiaa hii tuiache,” alisema.

Alimwomba mmoja wa viongozi wa dini aliyekuwepo eneo hilo kuongoza toba na baada ya kiongozi huyo kumaliza kuomba Rais Magufuli alisema amemsamehe OCD huyo.

“Ahsante sana baba (kiongozi huyo wa dini) na huyo OCD nimemsamehe abaki hapa hapa, yuko wapi huyo OCD…mwambie nimemsamehe kutokana na maombi haya,” alisema Rais Magufuli.

Aliwataka wananchi wa mkoa huo kuachana na vitendo vya ushirikiana na kuwaomba viongozi wa dini kuendelea kuhubiri matendo ya kweli kwa waumini wanaowaongoza.

Rais Magufuli pia alitoa rambirambi ya Sh milioni 5 kwa familia zilizopotelewa na watoto hao.

UJENZI WA STENDI

Rais Magufuli alionyesha kutoridhishwa na ujenzi wa stendi ya Mkoa wa Njombe ambayo ilianza kujengwa mwaka 2013 na hadi sasa haijakamilika na hivyo kutoa siku 30.

“Stendi imejengwa miaka lakini stendi za wengine zimekamilika kuna tatizo gani stendi ya Njombe isikamilike…watu wa Njombe wanashindwa kusafiri kwa sababu ya kuogopa kuchafuka kwa ajili ubovu wa stendi ya zamani,”alisema Magufuli.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Illuminata Mwenda, alisema kabla ya Juni stendi hiyo itakua tayari.

Alisema sababu ya kuchelewa stendi hiyo ni mkandarasi Masasi Constraction kushindwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

MKUU WA MKOA

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, alisema hivi sasa hali ni shwari na kwamba wote waliohusika na mauaji ya watoto wako mahakamani.

“Yale uliyoyasikia mwanzoni mwa mwaka huu tumeshughulikia yameisha na sasa tunaendelea kutoa elimu ili shetani aliyepita kuwashawishi watu kutoa roho za watu kwa misingi ya imani za kishirikina asirejee tena.

“Nakuomba radhi kwa kitendo hicho kilichotokea, nafanya toba nikiwa kiongozi na kwa niaba yao (wananchi),” alisema Ole Sendeka.

MAWAZIRI

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema Juni 2016 walipata Sh bilioni 3.2 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe unaofanywa na mkandarasi China Situan Internation Corporation. 

Alisema fedha za ujenzi huo zimetolewa na Serikali kwa asimilia 100 na kazi ya ujenzi imekamilika kwa asilimia 96 na kwamba wanatarajia kuanza kutoa huduma ifikapo Julai Mosi mwaka huu.

“Tutairejesha Hospitali Teule ya Rufaa ijulikanayo kama Kibena kwa Halmashauri ya Mji wa Njombe, tayari kuna watumishi 119 ambao tutawapanga katika hospitali hii,” alisema Ummy.

Hata hivyo alisema mpango wao ni kuhakikisha hospitali hiyo na nyingine za rufaa zinakuwa na madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, watoto, wanawake na wazazi, upasuaji wa jumla, upasuaji mifupa na ajali na wa mionzi.   

Waziri huyo pia alisema hivi sasa wanasomesha madaktari bingwa 311 katika vyuo mbalimbali na kwamba kila mwaka hupatiwa Sh bilioni 2.5 za ufadhili

“Madaktari bingwa hawa tumewafungisha mikataba wakimaliza lazima warudi kufanya kazi katika vituo na hospitali za Serikali kwa miaka mitatu kabla ya kwenda sehemu nyingine,” alisema.

Alisema pia wamepata Sh bilioni 2.2 kutoka Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Kifua Kikuu, Ukimwi na Malaria (Global Fund)kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.

Kuhusu dawa alisema awali Mkoa wa Njombe ulikuwa ukipata Sh milioni 459.9 lakini hivi sasa wanapata Sh bilioni 1.4 wakati Halmashauri ya Mji wa Njombe walikuwa wanapata kupitia Borahi Kuu ya Dawa (MSD) Sh milioni 44 lakini sasa wanapata Sh milioni 177.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema kitaifa mkoa huo unachangia asilimia 11.4 ya mazao ya chakula na kwamba baada ya kuunda kitengo cha masoko wamefanikiwa kupata masoko ya mazao mbalimbali likiwamo parachichi.  

Alisema pia wamepata soko kubwa la mahindi nchini Rwanda (tani 100,000), Burundi (100,000), Kenya na nchi nyingine za jirani ambazo zina mahitaji makubwa ya mahindi.

“Tumeondoa baadhi ya kodi kwa mbolea zinazoagizwa kutoka nje na mkakati wa muda mrefu tunaanzisha viwanda mbalimbali kwa ajili ya kuzalisha mbolea hapa nchini na tuna uhakika pembejeo zitakuwa na bei nafuu na wananchi watakuwa na uwezo wa kumudu,” alisema Hasunga.  

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, alisema mwaka 2015 upatikanaji wa maji Njombe ulikuwa asilimia 39 lakini baada ya kutekeleza miradi ya Sh bilioni 4.8 hivi sasa upatikanaji umefikia asilimia 67.2.

Alisema baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa kwa ushirikiano na Serikali ya India wenye thamani ya Sh bilioni 32.2 na miradi mitano ya thamani ya Sh bilioni 12.8 itamaliza tatizo lote la maji katika mji huo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema barabara ya Njombe – Moronga – Makete yenye kilomita 231 ni kiungo muhimu kinachounganisha makao makuu ya Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Mbeya hadi Uwanja wa Ndege wa Songwe.

Alisema barabara hiyo itaungwanishwa na ile ya Makambako – Songea hadi  Ziwa Nyasa sambamba na Bandari ya Mtwara.

Mbunge wa Njombe Mjini, wana changamoto kubwa za maji, barabara, utaalamu na ruzuku kwa ajili ya zao la parachchi.

“Mbao za Njombe tunafanya biashara mchana tu lakini usiku marufuku, tunaomba turuhusiwe kufanya biashara hii mpaka usiku,” alisema.

Alisema pia uwezo wa kiwanda cha maziwa ni zaidi ya lita 20,000 lakini hivi sasa kinazalisha lita 7,000 kutokana na kutokuwa na ng’ombe wenye uwezo wa kutoa maziwa ya kutosha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles