Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amemteua mke wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Salma Kikwete, kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilieleza kwamba uteuzi huo wa Salma ni kwa mujibu wa sheria na taratibu za kuapishwa kwake zitatangazwa na Bunge kwa mujibu wa utaratibu.
Uteuzi huo wa Salma ni wa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa kuwa mke wa kwanza wa Rais mstaafu kuteuliwa ubunge.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, leo (jana) amemteua Salma Kikwete kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Salma Kikwete ni mke wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete. Na ataapishwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zitakazotangazwa na Bunge,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu
Hadi uteuzi huo, Salma alikuwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), akitokea Wilaya ya Lindi.
Na katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alitajwa kuwa ni mmoja ya wana CCM watakaowania ubunge Jimbo la Lindi Mjini, lakini hakuweza kufanya hivyo licha ya kutakiwa na wana CCM wenzake.
Hata hivyo, mke huyo wa Rais mstaafu Kikwete anatajwa kuwa huenda akawania Jimbo la Lindi Mjini mwaka 2020.
Akizungumza na MTANZANIA kwa jana Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa CCM, Sophia Simba, alisema amefurahi kuona mpambanaji ameingia bungeni.
“Nimefurahi sana, Mama Salma Kikwete ni mpiganaji wetu wa masuala ya wanawake na maendeleo na amepambana sana kwenye masuala ya elimu, hasa kwa mtoto wa kike, kwenye kampeni ya mtoto wa mwenzio ni wako.
“Amesaidia kuongeza nguvu ya wanawake katika Bunge, naamini tutakuwa pamoja katika mapambano,’’ alisema Sophia.
Alisema uwezo mkubwa alio nao Salma ndani na nje ya Bunge, utasaidia kuimarisha na kupaza sauti za wanawake ndani ya Bunge kwa kuwa na nguvu.
“Salma ni mwanamke hodari na mwenye nguvu na aliye tayari katika kuipigania CCM pamoja na Serikali yake ili iweze kufanya kazi kama ilivyoaminiwa na wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Imani yangu mimi kama Mwenyekiti wa UWT, ninamshukuru sana Rais Dk. John Magufuli kwa kuendelea kuonyesha imani yake kwa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi,” alisema.
Salma Kikwete anakuwa ni mbunge wa nane wa kuteuliwa na Rais Magufuli katika nafasi zake 10 kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Hadi sasa wabunge walioteuliwa na Rais Magufuli ni Alhaji Abdallah Bulembo, Profesa Palamagamba Kabudi, Anne Malecela, Naibu Spika, Dk. Ackson Tulia, Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustino Mahiga, Profesa Makame Mbarawa (Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Dk. Philip Mpango (Fedha na Mipango).