30.8 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

RIPOTI YA TWAWEZA YAONGEZA HOFU HALI YA CHAKULA

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


WAKATI mjadala wa uhaba wa chakula ukiendelea nchini, Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Twaweza, imetoa ripoti ya utafiti inayoonyesha asilimia 69 ya kaya za Tanzania bara zinakabiliwa na uhaba wa chakula tangu mwaka 2016.

Ripoti hiyo inaonyesha asilimia 78 ya waliohojiwa wameripoti uhaba wa chakula katika maeneo wanayoishi, huku hali ikiwa mbaya zaidi vijijini ambako njaa inakadiriwa kuwapo kwa wastani wa asilimia 84 ikilinganishwa na mijini ambako ni asilimia 64.

Kwa mujibu wa Twaweza, utafiti huo uliotolewa jana na kupewa jina la ‘Uchungu wa Njaa’, ulifanyika katika mikoa yote ya Tanzania bara na kuhusisha watu 1,800 waliohojiwa Septemba 14-26 mwaka 2016 na wengine 1,610 waliohojiwa Februari 9-15 mwaka huu.

Ukusanyaji wa taarifa kutoka kwa watu hao ulifanywa kwa njia ya simu, ambayo kwa muda mrefu sasa imekuwa ikipingwa kutokana na kile ambacho wakosoaji wake husema wahojiwa hujibu kile watakacho wale wanaohoji kwa kuwa wanapewa simu bure.

Januari 16, mwaka huu, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, alisema hali ya chakula nchini si mbaya na kwamba Serikali haina mpango wa kugawa chakula bure kwa kuwa imefanya tathimini nchi nzima na kubaini hakuna uhaba huo.

Dk. Tizeba alitoa kauli hiyo baada ya viongozi mbalimbali wa kisiasa na kidini kutangaza kuwapo uhaba wa chakula, huku wakiitaka Serikali kuwajibika kwa kutoa chakula cha msaada.

Jana alipotafutwa ili azungumzie ripoti ya utafiti huo wa Twaweza, alisema kwa kifupi: “Usiniulize kuhusi ripoti ya Twaweza, bado sijaisoma.”

 

RIPOTI KWA UNDANI

Ripoti ya utafiti huo inaonyesha kuwa asilimia 51 ya kaya hazikuwa na chakula cha kutosha au mwanakaya kashinda na njaa kwa kukosa chakula.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema utafiti wao unaonyesha asilimia 69 za kaya nchini zinahofia kuishiwa chakula, huku asilimia 51 zikiripoti kutokuwa na chakula cha kutosheleza kaya nzima.

Utafiti huo pia unaonyesha asilimia 50 ya kaya zina mwanakaya aliyeshinda na njaa kwa sababu hakuweza kupata chakula.

Pamoja na mambo mengine, Eyakuze alisema jumla ya watu wanane kati ya kumi (asilimia 80) wameripoti kuwa kaya zao hazina kipato cha kutosha kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Kutokana na hali hiyo, Eyakuze alisema: “Upungufu na uhaba wa chakula unaoendelea ni kielelezo cha hali ngumu ya maisha iliyopo na umasikini wa kipato.”

Eyakuze alisema kwa mujibu wa wananchi wengi waliowahoji, uhakika wa kupata chakula umepungua kati ya Septemba 2016 na Februari mwaka huu.

Alisema kwa Februari, asilimia 65 ya watu waliohojiwa walikuwa na hofu ya kaya zao kukosa chakula ikilinganishwa na asilimia 45 waliosema hivyo Septemba mwaka jana.

Februari mwaka huu, asilimia 51 ya wananchi waliripoti kuna wananchi hawakuwa na chakula cha kutosha kwa ajili ya kaya zao katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

“Kabla ya hapo, Septemba mwaka jana, asilimia 43 ya wananchi waliripoti kuwa hali kama hiyo iliwatokea katika kipindi cha miezi 12 iliyopita,” alisema Eyakuze.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa asilimia 35 ya waliohojiwa  waliripoti kuwa na mwanakaya angalau mmoja aliyeshinda na njaa siku nzima kwa sababu ya kukosa chakula katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

“Hili ni ongezeko kutoka asilimia 21 walioripoti kwamba hali hiyo iliwatokea katika kipindi cha miezi sita tangu Aprili mpaka Septemba mwaka jana,” alisema Eyakuze.

Aidha alisema wahojiwa wa Sauti za Wananchi wameripoti kuwa kwa wastani kilo moja ya mahindi inawagharimu Sh 1,253.

 “Wananchi wamekumbwa na upungufu wa chakula. Tumepokea mwitikio wa Serikali katika suala hili na tunaunga mkono jitihada za kuzuia maafa makubwa.

“Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kwamba wananchi bado wanaishi kwenye hali ngumu na wamejaa hofu ya kukosa chakula. Jitihada za kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania yeyote anayelala njaa zishike nafasi ya kwanza katika vipaumbele vyetu vya kitaifa,” alisema Eyakuze.

 

MWAKILISHI UN

Akitoa tathmini yake kuhusu ripoti hiyo, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN), Alvaro Rodriguez, alisema visababishi vya mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kiasi chake vimesababisha upungufu wa mvua na utegemezi wa mvua katika sekta ya kilimo umesababisha hali kuwa mbaya zaidi.                                                                             

 “Lakini masuala ya upatikanaji wa chakula, unafuu na upatikanaji unapaswa kupewa kipaumbele wakati taifa likishughulikia tatizo hilo,” alisema Rodriguez.

 

ZITTO

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, alisema utafiti huo umethibitisha kile walichokuwa wakikipigia kelele kuhusu hali ya njaa nchini.

Alisema wanaendelea kutoa wito kwa Serikali kutangaza uwepo wa janga la njaa nchini na kuchukua hatua stahiki katika kuwapatia chakula cha dharura wananchi wote wanaokabiliwa na njaa.

“Ripoti hii inaonyesha kwamba takribani kati ya Watanzania 100 kati yao 50 kuna nyakati hawana chakula katika kipindi cha Septemba mwaka jana na Februari mwaka huu.

“Tangu Septemba mwaka jana, taarifa za Benki Kuu zilikuwa zinaonyesha tatizo hili, lakini hakukuwa na ‘action’ yoyote kutoka serikalini.

“Tangu Desemba mwaka jana watu walipozungumza kuhusu hali ya njaa, Serikali ikakataa na si Serikali tu hata Rais mwenyewe alikataa.

“Hakuna anayefurahia nchi ikiwa na njaa kwa sababu wanaoumia ni wananchi. Kinachoonekana sasa ni tatizo la kisera, haina maana kwamba miaka ya nyuma hapakuwa na tatizo hili isipokuwa Serikali zilizopita zilikuwa zina mfumo wa kuhifadhi chakula na kukiachia pale kunapokuwa kuna upungufu,” alisema Zitto.

Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, alisema jambo la chakula ni la usalama wa nchi, hivyo kitendo cha Serikali kukataa kujihusisha ni kukwepa jukumu lake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles