KHARTOUM, SUDAN
VIONGOZI wa kijeshi nchini hapa wametangaza makubaliano na muungano wa upinzani juu ya kipindi cha mpito cha miaka mitatu kwa ajili ya kukabidhi utawala wa kiraia.
Baraza hilo la kijeshi la mpito (TMC) lilisema jana kwamba muungano huo utakuwa na theluthi mbili ya viti katika Baraza la Bunge.
Sudan imekuwa ikitawaliwa na Baraza la Kijeshi tangu mwezi uliopita baada ya mapinduzi ya Rais Omar al-Bashir.
Tangu kipindi hicho maandamano yaliyosababisha kuanguka kwa utawala wake yamekuwa yakiendelea, huku waandamanaji wakidai kuwekwa kwa Serikali kamili ya kiraia.
Saa kadhaa kabla ya mkataba wa sasa kutangazwa, takriban waandamanaji watano na ofisa mmoja wa usalama waliuawa katika makabiliano mjini hapa.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Luteni Jenerali Yasser al-Atta alisema makubaliano ya mwisho juu ya mgawanyo wa madaraka yatasainiwa pamoja na upinzani (DFCF) katika kipindi cha saa 24 kuanzia jana na yatajumuisha kubuniwa kwa baraza la kujitawala ambalo litaongoza taifa hadi uchaguzi utakapofanyika.
“Tunaapa kwa watu wetu kwamba makubaliano yatakuwa yamekamilika katika kipindi cha saa 24 kwa njia inayotarajiwa na watu,” alisema.
Jenerali Atta alisema kuwa DFCF itakuwa na theluthi mbili ya viti 300 vya bunge la mpito huku viti vilivyosalia vikichukuliwa na vyama ambavyo si sehemu ya muungano wa upinzani.
Awali, msemaji wa vuguvugu la waandamanaji, Taha Osman alisema kuwa pande zote zimekubaliana juu ya muundo wa mamlaka zijazo za utawala ambazo ni Baraza la Utawala, Bunge na Baraza la Mawaziri.
Kwa upande wake, Mjumbe wa DFCF, Satea al-Hajj alielezea matumaini yake kuwa yaliyomo katika mkataba wa mwisho juu ya mgawanyo wa madaraka yatakubaliwa.
“Maoni yamekubalika na kwa mapenzi ya Mungu tutafikia makubaliano karibuni,” alisema.
Awali jeshi lilitaka kipindi cha mpito cha miaka miwili huku kiongozi wa waandamanaji alitaka kipindi cha mpito kiwe cha miaka minne.