Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
KIKOSI cha timu ya Yanga, leo kinatarajia kuelekea mkoani Njombe, kwa ajili ya mchezo wake dhidi ya Njombe Mji utakaopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Sabasaba.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara watawavaa Njombe Mji wakiwa na kumbukumbu ya kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli FC, kwenye mchezo wao wa ufunguzi uliopigwa kwenye Dimba la Uhuru, Dar es Salaam.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten, alisema kikosi chao kitaondoka kuelekea Njombe kikiwa na wachezaji 26.
“Timu itafanya mazoezi yake ya mwisho leo (jana) jioni na kesho (leo) itaondoka kuelekea Njombe.
Msafara utakuwa wa wachezaji 26 isipokuwa Amiss Tambwe, Beno Kakolanya na Baruhani Akilimali ambao bado wanaendelea na matibabu,” alisema.
Alisema wanatarajia mchezo huo utakuwa ni mgumu ukizingatia watakuwa ugenini, lakini watahakikisha wanavuna pointi tatu muhimu.
Wakati huo huo daktari wa timu hiyo, Edward Bavu, alisema wachezaji wao, Obrey Chirwa, Geofrey Mwashiuya wanaendelea na mazoezi mepesi huku wakitarajiwa kuungana na wenzao kwenye msafara utakaoelekea Njombe.
“Kwenye mazoezi ya leo (jana) jioni ntaendelea kuwaangalia hawa majeruhi, lakini hali zao hadi sasa zinaendelea vizuri isipokuwa Tambwe, Akilimali na Kakolanya ambao watabaki Dar es Salaam kwa matibabu zaidi,” alisema.