Na MALIMA LUBASHA,
MAHAKAMA ya Wilaya ya Serengeti imewahukumu watu watatu kifungo cha miaka 73 jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kuingia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuua tembo.
Hukumu hiyo ilitolewa Desemba 9 mwaka huu na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Emmanuel Ngaile wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti.
Alisema adhabu hiyo imetolewa kutokana na kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Waliohukumiwa kutumikia adhabu hiyo jela ni Augen Nicodem (41) mkazi wa Mkoa wa Kigoma, Mwita Marwa (27) na Amos Alexender (25), wote wakazi wa Wilaya ya Serengeti.
Hakimu Ngaile alisema katika kosa la kwanza la kuingiza na bunduki ndani ya hifadhi kinyume cha sheria za nchi kwa ajili ya kufanyia vitendo vya ujangili mahakama imewahukumu watumikie adhabu ya miaka 15 jela.
Alisema kosa la pili la kusafirisha silaha kutoka Burundi hadi Tanzania kinyume na kifungu namba 18 cha sheria ya mlipuko ya mwaka 2002 ambalo walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.
“Katika kosa la tatu la kupatikana na silaha ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kinyume cha Sheria ya Hifadhi ya Taifa ya mwaka 2002 watatumikia kifungo cha miaka miwili kila mmoja.
“Kosa la nne la kuingia ndani ya hifadhi bila kibali washtakiwa watumikia kifungo cha mwaka mmoja kila mmoja na kosa la tano la kuua Tembo ndani ya hifadhi adhabu yake ni miaka 10,” alisema.
Alisema kwa kosa la sita la kupatikana na nyara za serikali kinyume cha sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 washtakiwa walihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30.