33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jela miaka 60 kwa kubaka mwanafunzi

 WALTER MGULUCHUMA– KATAVI

MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemuhukumu mkazi wa Mtaa wa Msasani, Kata ya Mpanda Hotel, Manispaa ya Mpanda, Said Selemani (20), kifungo cha miaka 60 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari ST Mary. 

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Gospher Luhoga, baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi nane, akiwemo msichana mwenyewe aliyefanyiwa kitendo hicho na daktari aliyemfanyia uchunguzi, wakati mshtakiwa hakuwa na shahidi hata mmoja na upande wa mashtaka uliongozwa na mwanasheria wa Serikali, Grogory Mhangwa. 

Awali kwenye kesi hiyo, mwendesha mashtaka wa Serikali, Mhangwa aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kwa wakati tofauti Novemba 23, 2019 na Desemba 4, 2019 katika Mtaa wa Msasani. Alidai mshtakiwa alimtorosha mwanafunzi huyo na kisha alimbaka kwa nyakati tofauti na Desemba 4, mwaka jana alikamatwa na polisi saa tano usiku. 

Katika utetezi wake mahakamani hapo, mshtakiwa alidai kuwa siku hiyo wakati alipokamatwa akiwa na mwanafunzi huyo, alikuwa amefika nyumbani kwake ili aweze kumsaidia kumpeleka nyumbani kwao kwa kuwa alikuwa amefukuzwa na wazazi wake. 

Alidai wakati wakiwa ndani na mwanafunzi huyo akijiandaa kumpeleka kwa wazazi wake, ndipo alipokamatwa na polisi.

Hakimu Mkazi Luhoga baada ya kusikiliza pande zote mbili, alisema kutokana na ushahidi uliotolewa, mahakama imemwona mshtakiwa ana hatia ya kumbaka mwanafunzi huyo. 

Alitoa nafasi kwa mshtakiwa kama anayo sababu yoyote ya msingi ambayo inaweza ikaifanya mahakama iweze kumpunguzia adhabu. 

Katika utetezi wake, mshtakiwa aliomba mahakama imwonee huruma kwa kumpunguzia adhabu kwa kuwa kuna familia inamtegemea na pia bado umri wake ni mdogo. 

Utetezi huo ulipingwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mhangwa, ambaye aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwa kuwa matukio ya watu kubakwa yamekuwa yakijirudia mara kwa mara katika mkoa huo.

Hakimu Luhoga baada ya kusiliza pande hizo mbili alisema makosa yaliyomtia mshtakiwa hatiani yanakiuka Sheria ya Elimu Namba 133 sura 16 ya marejeo ya 2002 na sheria Namba 131(1) (2) (e) na 131 (1) sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002. 

Alisema adhabu yake ni kila kosa kifungo cha miaka 30 na huwa hakuna adhabu nyingine tofauti na kifungo hicho kwa mtu aliyepatikana na hatia hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles