SEOUL, KOREA KUSINI
JARIBIO jipya la Korea Kaskazini kurusha kombora limeshindikana baada ya kuripuka muda mfupi tu lilipofyatuliwa jana, ikiwa ni siku moja tangu ilipoonesha hazina yake ya makombora katika gwaride kubwa la kijeshi.
Kushindwa huko , ambako kunaonekana kwa umma kama kitu cha fadhaa kwa serikali ya nchi hiyo, kumekuja huku hali ya wasi wasi ikiongezeka katika rasi ya Korea kuhusu dhamira ya taifa hilo kujipatia silaha za nyuklia.
Hata hivyo haikuwezekana kufahamika mara moja aina gani ya kombora hilo.
Jaribio hilo limekuja baada ya Korea Kaskazini kuonesha karibu makombora 60 ikiwamo jipya lenye uwezo wa kuvuka mabara wakati wa gwaride siku ya Jumamosi kuadhimisha miaka 105 ya kuzaliwa kwa mwasisi wa taifa hilo, Kim II-Sung.
Sherehe hizo zilifanyika mbele ya kamera za mashirika ya habari duniani yaliyoalikwa na ambayo yalikuwapo pia wakati wa jaribio la kurusha kombora hilo lililoshindwa.
Aidha kushindwa kwa kombora hilo kunakuja saa chache kabla ya ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence nchini hapa, ambako suala la Korea Kaskazini litakuwa ajenda ya juu.
Korea Kaskazini ina tabia ya kurusha makombora kuadhimisha sherehe muhimu za kisiasa, ama kama ishara ya ukaidi wakati maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani wanapofanya ziara eneo hilo.