Tunu Nassor -Dar es salaam
JAMII imeshauriwa kuzungumza na watoto wao kuanzia wakiwa tumboni ili kukuza ubongo wao na kuwajengea uwezo wa kuelewa mambo wakiwa bado wadogo.
Akizungumza wakati wa mkutano wa siku mbili wa kujadili ukuaji na maendeleo ya watoto wakiwa hatua za awali, Dar es Salaam jana, mtafiti kutoka Taasisi ya Ubongo Learning, Aneth Ngongi alisema mtoto anaanza kujifunza mambo mengi tangu akiwa tumboni.
“Mtoto angali tumboni ana uwezo wa kujifunza mambo mengi yaliyopo duniani kupitia kusikia na hisia, ni vema kwa wazazi kuanza kuongea na kucheza naye katika kipindi hicho,” alisema Aneth.
Alisema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuukuza ubongo wa mtoto na kuwa mwerevu akiwa na umri mdogo.
Aneth alisema taasisi hiyo imekuja na mfumo wa kidigitali wa kujifunzia elimu kwa watoto ambao utawasaidia kujifunza kupitia katuni na kucheza.
Alisema ni vema wazazi kuanza kuweka mazingira bora ya kujifunzia kwa watoto wawapo wadogo kwa kuchagua maudhui ya kuelimisha.
“Ubongo Learning tuna nafasi kubwa ya kuzifikia familia nyingi barani Afrika kupitia simu na kutoa ujumbe wa kuelimisha na kuweza kubadilisha maisha yao, hivyo ni jukumu la wazazi kupokea maudhui yetu,” alisema Aneth.
Alisema taasisi hiyo imekuwa na vipindi vya luninga vyenye mafunzo mbalimbali kwa watoto kulingana na umri wao.
“Katika vipindi, tumeongeza kipande cha wazazi kinachoitwa ‘tunakujenga’ ambapo tunawakumbusha wazazi wajibu wao katika malezi bora ya watoto,” alisema.