Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Dyansobela katika shauri No. 28/2017 leo tarehe 31/03/2017 imetoa amri dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi kumzuia Prof Lipumba kutoa fedha za Ruzuku ya Chama cha Wananchi- CUF mpaka shauri namba 21/2017 dhidi ya Msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu kutoa fedha za ruzuku shilingi milioni 369 kwa njia za wizi na udanganyifu litakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.
Amri hiyo ya Mahakama Kuu imekuja baada ya Jopo la Mawakili wa Chama wanaoiwakilisha Bodi ya Wadhamini ya CUF ambao ni Mhe. Juma Nassor, Mhe Daimu Halfani na Hashim Mziray kuwasilisha maombi hayo mbele ya Mahakama Kuu kuiomba kutoa amri hiyo kwa kuwa fedha zilizotolewa awali milioni 369 hazijulikani zimetumika vipi, na hazikuwa katika mikono salama wala hakuna udhibiti wowote wa Chama –CUF juu ya fedha hizo ikizingatiwa kuwa Lipumba alishavuliwa Uanachama.
Hata hivyo Wakili Juma Nassor aliyewasilisha maombi hayo aliweka mkazo na kusisitiza kuwa kwa mazingira yaliyopo ni vyema na Busara kwa fedha za umma zilizopaswa kutolewa kama Ruzuku kwa Chama Cha CUF kwa sasa ziendelee kubaki serikalini.
Jaji Dyansobela amekubaliana na hoja zote.