29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

LIJUALIKALI ASIMULIA MATESO YA GEREZANI

Na ASHA BANI

MBUNGE wa Jimbo la Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali, amesema licha ya mateso makali aliyoyapata akiwa gerezani lakini amefurahia kifungo hicho kwani kimempa heshima kubwa.

Amesema anaona ni heshima kwa kuwa amefungwa kwa ajili ya kutumikia kura ambazo alizipata katika uchaguzi mkuu uliopita na kwa sababu hiyo ni kama amepata shahada ya udaktari (PhD).

Lijualikali ambaye aliachiwa huru juzi na Mahakama Kuu ambayo ilitengua kifungo cha miezi sita jela iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya  Kilombero,  aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kutoka nje ya lango la Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam alikokuwa akitumikia kifungo hicho.

Kuhusu mateso aliyoyapata akiwa kifungoni, alisema yeye na wenzake walikuwa wanafanyiwa vitendo vya kikatili ikiwa ni pamoja na kupigwa na rungu lililobatizwa jina la ‘Trump’.

Akielezea hali ya ubaya wa chakula cha gerezani alitolea mfano wa chakula cha dagaa ambao iwapo wakioshwa kiwango cha mchanga ni nusu kikombe.

“Tulikuwa tunakula ugali wa dona ambao kwa mtu wa kawaida huwezi kula kwa sababu umechanganywa na magunzi,” alisema.

Alisema ndani ya gereza hilo kuna eneo linaitwa Sitaki Shari ambalo hutumika kutesea wafungwa.

Akishuhudia alisema alimwona mfungwa mwenzake ambaye alipigwa katika eneo hilo kiasi cha kutambaa.

Akizungumzia uhusiano wake na maofisa wa magereza, alisema kitaasisi ulikuwa ni mbaya japo kwa askari mmoja mmoja alikuwa akizungumza nao pasipo shida.

Akifafanua alisema kwa hadhi yake yeye kama mbunge alipaswa kulazwa daraja la tatu ingawa aliwekwa katika eneo tofauti na kuliacha daraja hilo wakilazwa watoto wa viongozi, watuhumiwa wa meno ya tembo na raia wa China ambao hakusema walikuwa wanatuhumiwa kwa kesi gani.

“Magereza kuna madaraja matatu, la kwanza, pili na la tatu ambalo nilitakiwa kulazwa humo ili nipewe ulinzi kutokana na hadhi yangu,” alisema.

Alisema vitendo hivyo na vingine ambavyo hakuvisema atavipeleka ndani ya Bunge Dodoma.

Awali, Lijualikali alieleza kile alichokitaja kuwa ni sababu za kifungo hicho akisema ni msimamo wake wa kukataa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchakachua kura kwenye uchaguzi wa Halmashauri ya jimbo hilo.

Alisema msingi hasa wa kifungo hicho ni uhuni na udhalimu uliofanywa na chama hicho dhidi yake kwa kuwa kisheria alitakiwa kuruhusiwa kupiga kura kwa maana yeye ni mbunge halali aliyechaguliwa na wananchi.

Alisema kuzuiwa kwake na CCM ni kutokana na kujua kwamba kama  angeruhusiwa kupiga kura angeyafanya matokeo yakawa mabaya kwa upande wao.

“Baada ya kufanya uhuni na udhalimu wao wakaamua kunipa na kesi kwa madai kuwa nimefanya vurugu lakini kwa misingi hiyo ya kutetea, kupigania na kupinga udhalimu uliokuwa ukifanywa na CCM,” alisema.

Alihoji kama yeye ambaye ni Mbunge mwenye hadhi ya kidiplomasia katika nchi anaweza akafanyiwa huo aliouita uhuni wa kutungiwa mashtaka ya uongo ili kukidhi matakwa ya CCM, kwa mwananchi wa kawaida hali ikoje?

 “Niliwahi kuwaambia wabunge wenzangu wasivae uhusika kuwa wao wa daraja fulani la juu kwa kuwa ni wabunge kama mimi mbunge mwenzao nimefanyiwa hivi wao ni akina nani hasa? Tuungane kupinga.”

Mbali na hilo, Lijualikali aliwalaumu wale aliowaita kuwa ni wenye hekima kukaa kimya kwa kitendo kilichomkuta.

KUHUSU NAPE

Lijualikali pia alitumia fursa hiyo kueleza mshangao wake wa tukio la aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kulisimamisha Taifa kwa sababu tu ya kutishiwa bastola.

Katika hilo alisema yeye ametishiwa mara nyingi bunduki ikiwamo kichwani tena hadharani lakini wenye hekima zao wakakaa kimya.

 “Jambo dogo tu bastola nchi nzima inalalamika halafu Nape anasema vijana wasikate tamaa, nani anakata tamaa sisi au wao ambao wameanza sasa?” alihoji mbunge huyo.

AKUMBUSHA MACHUNGU YA 2015

Katika hatua nyingine mbunge huyo alikumbusha machungu ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 jinsi Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, kukata jimbo lake.

“Nitawaelezea vizuri, Lubuva alipokuja jimboni na alichokifanya yaani mfano rahisi ni kama jimbo la Kinondoni na Ubungo, halafu kata zote kumi zimewekwa Kinondoni na kumi Ubungo pale katikati ndio jimbo langu mimi nikagombee ni hatari sana,” alisema Lijualikali.

SUMAYE

Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema nchi kwa sasa ipo ‘labour’ kutokana na machungu waliyonayo Watanzania.

Alisema hakuna mtu asiyefahamu ili mwanamke apate mtoto lazima apate uchungu ajifungue tena kwa uchungu na jinsi uchungu unavyozidi ndio mtoto anakaribia kuzaliwa.

“Kwa sasa demokrasia ya nchi ipo ‘labour’ na mtoto ni lazima apatikane basi kila Mtanzania asikate tamaa ushindi wa demokrasia lazima utapatikana, msiogope tusimame kifua mbele tutashinda,” alisema Sumaye.

Aliongeza kuwa Mahakama za chini zimeshindwa kufanya kazi zake inavyotakiwa na matokeo yake zinafanya kazi kwa kuagizwa kutoka mamlaka za juu na kutaka hali hiyo isifumbiwe macho.

Alisema kwa sasa waliobakia wakipiga kelele zakupinga vitendo vya uonevu dhidi ya Serikali imebakia Chadema na CUF wamewaingiza katika mgogoro ili kuwazoofisha jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa demokrasia nchini.

“Mateso wanayotupatia yanatakiwa kuimarisha wananchi na si kuwanyong’onyeza tutashinda tu, mfano mzuri aliyekuwa Rais wa Libya, Muammar Gaddafi, alikuwa na jeshi kubwa lakini kiko wapi?” alihoji  Sumaye.

 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles