COLOMBO, SRI LANKA
IDADI ya watu waliofariki dunia kwa shambulio la mabomu ya kujitoa muhanga wakati wa Sikukuu ya Pasaka nchini hapa imeongezeka na kufikia 359.
Taarifa hiyo ya polisi imekuja wakati viongozi wa nchi hii wakiapa kufanyia mabadiliko vyombo vya usalama kutokana na mapungufu katika intelijensia kabla ya shambulio hilo.
Viongozi hao walisema baadhi ya vikosi vya usalama vilifahamu kabla ya Pasaka kuhusu uwezekano wa mashambulizi, lakini havikusambaza taarifa hizo za tahadhari katika sehemu kubwa.
Wakati huo huo Balozi wa Marekani nchini hapa, Alaina Teplitz , amewaambia waandishi habari kuwa bila shaka kulikuwapo na hali ya kushindwa kwa mfumo.
Teplitz alisema Marekani haikuwa ikifahamu kabla kuhusu kitisho cha shambulio kabla ya kutokea.
Alisema timu ya wapelelezi wa Shirika la Upelelezi Marekani (FBI) na maafisa wa jeshi la Marekani walikuwa wanasaidia katika uchunguzi huo.