25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Hoja tano zilizombeba Dk. Mwinyi urais Z’bar

 FREDY AZZAH Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemchagua Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea wake wa urais Zanzibar baada ya Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) kumchagua kwa kura 129 sawa na asilimia 78.65. 

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, wajumbe wote wa NEC ni 167 lakini waliohudhuria kikao cha jana na kupiga kura walikuwa 166. 

Kati ya wajumbe waliopiga kura hizo, 68 wanatoka Zanzibar, hivyo kwa ujumla Mwinyi kachaguliwa na idadi kubwa ya kura kutoka Zanzibar kwani washindani wake kwa ujumla wao walipata kura 35. 

Mbali na wingi wa kura hizo ambao umeondoa dhana ya kwamba Rais wa Zanzibar anachaguliwa na Bara, pia katika kikao kilichofanyika mjini Dodoma jana, Mwinyi alionekana kubebwa zaidi na hoja tano huku washindani wake alioingia nao kwenye tatu bora wakionekana kuanza kushindwa kuanzia wakati wa kujieleza. 

Wagombea walioingia tatu bora na Mwinyi ni Shamsi Vuai Nahodha aliyepata kura 16 sawa na asilimia 9.75 na Dk. Khalid Salum Mohammed ambaye alipata kura 19 sawa na asilimia 11.58.

Jana baada ya Rais Dk. John Magufuli kufungua kikao, wagombea wote watano ambao walipitishwa na Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya CCM iliyokaa Zanzibar kabla ya kuchujwa juzi na Kamati Kuu na kubaki watatu, waliruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa mkutano. 

Katika kikao hicho, Profesa Makame Mbarawa na Khamis Mussa Omar, ambao waliishia kwenye tano bora baada ya majina yao kuenguliwa na Kamati Kuu ya chama hicho, walipata nafasi ya kuzungumza na wote kuahidi kushirikiana na yeyote ambaye angeshinda. 

USHINDI WA MWINYI 

Kwa mujibu wa katiba ya CCM, mshindi ilikuwa lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zitakazopigwa na baada ya wagombea kupewa nafasi ya kujieleza, ushindi wa Dk. Mwinyi ulionekana Dhahiri.

Licha ya kwamba Dk. Mwinyi alijieleza kwa muda mfupi ikilinganishwa na wenzake, lakini alionekana kuwa mtu anayechagua kila neno alilotamka. 

Mbali na kueleza wasifu wake, Dk. Mwinyi wakati akiomba kura alijikita zaidi kuahidi kulinda Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na muungano huku pia akisema ataendeleza yote yaliyofanywa na watangulizi wake hasa awamu ya saba iliyoongozwa na Dk. Mohammed Shein. 

Pia Mwinyi alisema chama hicho kikimpa ridhaa ya kupeperusha bendera yake, atasimamia kwa vitendo ilani ya chama chake atakayokabidhiwa. 

“Ahadi yangu kwenu, endapo mtanichagua nitayaezi mapinduzi ya mwaka 1964 ya Zanzibar na nitadumisha muungano wetu, pia nitaendeleza yale yote mazuri yaliyofanywa na awamu zilizotangulia hasa awamu ya saba chini ya Dk. Ally Mohamed Shein. 

“Vilevile niahidi kwamba nitaitekeleza kwa vitendo ilani ya mwaka 2020/2025 ambayo itatolewa kwa upande wa Zanzibar, kwa heshima na taadhima naomba mnipigie kura za ndiyo,” alisema Mwinyi. 

Wakati Mwinyi akijieleza muda wote wajumbe wa kikao hicho walionekana watulivu huku, baadhi wakinong’ona kuwa Nahodha anaweza akajieleza vizuri zaidi. 

 Wa pili kujieleza alikuwa ni Nahodha ambaye mbali na kuwahi kuwa Waziri Kiongozi pia mwaka 2010, aliwania nafasi hiyo na kuchuana na Dk Shein ambaye anamaliza muda wake. 

Tofauti na ilivyotazamiwa, hotuba yake haikuonekana kuwakuna wajumbe kwani alijikita zaidi kuzungumza alivyosaidiwa na Dk. Shein hata wakati ambapo wasaidizi wake walionekana kuwa kikwazo. 

Dk. Khalid naye alionekana kujieleza vyema ingawa baadhi wanasema pamoja na mambo mengine, kutokaa kwenye chama kwa muda mrefu kunaweza kuwa sababu ya kutopewa nafasi kubwa. 

Mgombea huyu aliyeibuka wa pili, mbali na kufanya kazi kwenye Serikali kwa muda mrefu katika siasa na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla aliingia rasmi mwaka 2016. 

MWINYI ASHUKURU 

Baada ya upigaji kura kukamilika, Mwinyi alipata fursa ya kutoa neno la kushukuru ambapo pamoja na mambo mengine alisema amepata heshima kubwa na kura alizopata ni nyingi na kuahidi kutumikia taifa lake kwa moyo wake wote. 

“Kwenye maisha yangu nimefanya mitihani mingi, lakini mkubwa kuliko yote ni huu (mchakato wa CCM), nafarijika kuwa timu hii ya NEC tutakuwa pamoja katika kutafuta ushindi wa CCM,” alisema Mwinyi.

Mwinyi pia alishukuru wenzake na kusema sasa timu zote zimekufa na sasa jambo kubwa ni kuhakikisha ushindi wa CCM unapatikana kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba.

MARAIS WAKANA WAGOMBEA 

Wakati kikao kikiendelea, Rais Magufuli na Dk Shein walisema wamekuwa wakihusishwa na baadhi ya wagombea kuwa wanawaunga mkono jambo ambalo walisema si kweli.

Rais Magufuli alisema amehusishwa na kumtuma Profesa Mbarawa, jambo ambalo si la kweli na mgombea huyo ameishia kwenye tano bora.

“Sijui sasa mtasema niko na nani,” alisema Rais Magufuli.

Naye Dk. Shein alisema alihusishwa na Dk. Khalid kitu ambacho si cha kweli na kwamba hajawahi kuwa na mgombea na kamwe hatokuwa naye.

Katika hatua nyingine kikao cha jana kimempitisha pia Rais Magufuli kuwa mgombea wa urais wa Tanzania ambaye leo ataidhinishwa na Mkutano Mkuu wa 10 wa chama hicho.

Kabla ya kupitishwa, Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alitoka nje ya mkutano na nafasi yake kushikwa na Dk Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti.

Dk. Shein aliwaongoza wajumbe kupitisha jina la Rais Magufuli ili amalizie muhula wake wa pili jambo ambalo lilikubaliwa kwa kauli moja.

Akizungumza baada ya NEC kumpitisha, Rais Magufuli mbali na kushukuru kwa nafasi hiyo, pia aliwataka Wazanzibar kuwa wamoja na kuhakikisha wanajenga uchumi wa nchi hiyo.

Aliwataka wapuuze maneno ambayo yamekuwa yakizungumzwa kwani bila CCM imara hakuna maendeleo Zanzibar.

“Yatazungumzwa maneno mengi bila CCM imara hakuna maendeleo, Zanzibar ni tajiri na mabeberu wanaitamani na bila muungano hakuna Pemba wala Unguja simamieni uimara kujenga umoja.

“Tumtangulize Mungu kwenye kila jambo hata mimi sikuja kwamba nitakuja kuwa Rais kila mmoja na zama zake,”alisema

WATU 2400 KUHUDHURIA MKUTANO

Katika hatua nyingine Katibu wa Itikadi na Uenezi,Humphrey Polepole alisema kwamba jumla ya watu 2400 wanatarajiwa kuhudhuria katika Mkutano Mkuu wa kumi wa chama hicho unaotarajia kufanyika leo na kesho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles