25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

CCM yamsamehe Kinana, yabariki Membe kufukuzwa

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kumsamehe aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abrahaman Kinana huku kikimchinjia baharini aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.

Uamuzi huo umetangazwa jana jijini hapa na Mwenyekiti wa chama hicho tawala, Dk. John Magufuli wakati akiendesha mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanyika katika Ukumbi wa White House.

Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  alisema mapendekezo ya kikao yalipendekeza Kinana apewe adhabu kwa muda wa miezi 18.

Alisema mpaka sasa ametumikia adhabu hiyo kwa miezi mitano ambapo alisema Kinana alimgusa kutokana na kuomba radhi hadharani.

“Kikubwa aliomba radhi hadharani kwa kweli amenigusa sana, CCM ni chama chenye huruma niwaombe ndugu yetu huyu tumsamehe, mnasemaje tumsamehee….,”alisema Magufuli huku wajumbe wakisema tumsameheeee.

Aidha, mwenyekiti huyo alimwagiza Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally kumwalika leo katika Mkutano Mkuu wa 10 wa chama hicho.

“Nimemwagiza Katibu Mkuu amwalike kesho (leo) Kinana na viongozi wetu wastaafu, CCM kinapenda viongozi wanyenyekevu na hakuna malaika,”alisema Rais Magufuli.

Kuhusiana na Membe, Rais Magufuli alisema: “Yule mwingine sina sababu ya kumtaja ameishajiondoa moja kwa moja,”alisema.  

WAANDISHI WARUHUSIWA KWA MARA YA KWANZA

Katika hatua nyingine Dk. Magufuli aliruhusu waandishi kuhudhuria kwa mara ya kwanza kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho huku akidai kwamba demokrasia ndani ya chama hicho ni kubwa.

Mara baada ya zoezi la ufunguzi wa mkutano huo kukamilika Dk. Bashiru aliwataka waandishi watoke nje lakini mwenyekiti wake alitoa maagizo kwamba waandishi wabaki kwa ajili ya kuripoti tukio hilo.

ILANI IJAYO KUTOA AJIRA MILIONI SABA KWA VIJANA

Dk. Bashiru alisema ilani ijayo ya CCM lengo lake ni kuendelea kustawisha uchumi wa Mtanzania na Taifa kufikia uchumi wa kati ambao tayari Serikali imeishaufikia.

“Ili tuendeleza haya CCM katika miaka mitano ijayo na Serikali zake italinda utu, usawa na kudumisha amani pamoja na mshikamano, pili ni kukuza uchumi wa kisasa na fungamanishi jumuishi na shindani uliojengwa katika misingi ya viwanda pamoja na kuleta mapinduzi ya chakula.

“Pia kukuza uchumi wa kisasa jumuishi na shindani uliojengwa katika misingi ya viwanda na kuleta mapinduzi ya kilimo pamoja na kutengeza ajira sizizopungua  milioni saba katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana wetu,”alisema Dk. Bashiru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles