MWAKA jana wakati wa kipindi cha kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, mambo mengi sana yalikuwa yanaendelea hapa nchini. Wakati huo, kama ilivyo sasa, ilikuwa rahisi sana kwa watu kupata taarifa za matukio mbalimbali yanayotokea wakati huo huo, kwa kutumia simu zao za mkononi.
Wakati hayo yakitendeka, mambo yaliyokuwa yakitumwa kupitia simu hizo za mkononi yalikuwa ya ajabu sana, kiasi cha kukera. Kuna wakati niliwahi kuandika katika safu hii hii, kwamba Watanzania tuna ushamba wa mitandao ya jamii. Hii ilikuwa baada ya watu kuitumia kutuma mambo ya ajabu kama vile picha za maiti, wakati ni kinyume cha maadili.
Nakumbuka kauli yangu hiyo ilitokana na kitendo cha watu kutuma picha ya mwili wa Kapteni John komba uliokuwa kitandani hospitali, baada tu ya kutangazwa kwamba amefariki. Kupiga picha mwili ule na kisha kuusambaza kwenye mitandao ya jamii bila hata kujali familia yake na namna ambavyo wangependa mpendwa wao asitiriwe, lilikuwa jambo la kukera sana.
Bado Watanzania tulifikia hatua ya kupiga picha za maiti wa ajali mbalimbali zilizokuwa zikitokea na kuirusha moja kwa moja kwenye mitandao ya jamii kupitia simu za mkononi. Hatukujali staha ya marehemu, hatukujali kama ndugu wa marehemu wameshapata habari ama la, hatukujali hata wengine ambao wangeona picha zile, kama kweli walihitaji kuziona katika hali ile. Ilisikitisha sana.
Lakini sasa inaelekea ushamba huo umeanza kuondoka kidogo na sasa mitandao ya jamii inatumika kwa njia sahihi, pengine ambayo ilikuwa imekusudiwa tangu awali. Katika kipindi kifupi sana, matumizi ya mitandao ya jamii hapa nchini yamesaidia kuibua wala rushwa; yamesaidia kuibua walevi wa madaraka waliojaribu kutumia vyeo vyao ama vya wenzi wao kukwepa kuadhibiwa walipokuwa wamekosea na sasa yamesaidia hata kuonyesha vitendo visivyostahili ambavyo vinafanywa na walimu dhidi ya wanafunzi.
Wenzetu wa Tunisia walifanikiwa kumng’oa Rais wa nchi yao kupitia mitandao ya jamii. Arab Spring ilianza pale mchuuzi wa matunda mtaani, Mohamed Bouazizi, alipojichoma moto mwaka 2011. Binamu zake walitumia mitandao ya jamii kurusha kipande cha video kilichomwonyesha mama yake akiongoza maandamano na kuelezea namna mwanae alivyonyanyaswa na askari, wakati biashara aliyokuwa akiifanya ilikuwa ikimlisha mama huyo na watoto wake wengine.
Watazamaji walikasirishwa na manyanyaso yale na waliungana na familia ya Bouazizi kuandamana kupinga unyanyasaji dhidi ya wananchi na ndani ya siku 28, Rais Ben Ali aliyekuwa amekaa madarakani kwa miaka 24, aling’olewa. Hiyo ilikuwa nguvu ya mitandao ya jamii ambayo ilitumiwa vizuri kufikisha ujumbe na hata kuhamasisha wananchi kupinga manyanyaso yaliyokuwa yakifanywa dhidi yao.
Misri nayo hali ilikuwa hivyo hivyo, baada ya picha za kijana mmoja aliyeuawa kutokana na kipigo cha polisi, kusambazwa. Ilifikia hatua, ukaanzishwa ukurasa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, ulioitwa We are all Khaled Saeed. Wananchi waliandamana na waliitumia mitandao ya jamii kuhamasishana kuhakikisha kwamba uonevu dhidi yao unakwisha. Mwisho wa siku, Rais Hosni Mubarak ambaye alikuwa ametawala Misri kwa miaka 30, aling’oka.
Hapa, najaribu kusisitiza umuhimu wa kuitumia mitandao ya jamii vizuri kwa ajili ya kuleta haki, na kuficha uozo kama ambavyo kwa Tanzania, sasa hivi tumeanza kuona matunda yake.
Ni kweli kwamba bado tuna safari ndefu ya kukubali kwamba mitandao hii haitakiwi kutumika kutukana watu, kuzusha mambo ya uongo au hata kuhamasisha uvunjifu wa amani. Safari bado ni ndefu sana na licha ya kwamba huwezi kudhibiti kila lililo ovu, upo mwanga wa matumaini.
Tuendelee kufichua maovu, tuendelee kutetea watoto, tuendelee kufichua wabakaji na tundelee kuwaumbua wale wanaolichafua jina la nchi yetu kwa kuomba na kupokea rushwa za shilingi elfu sitini. Hivi ndivyo mitandao ya jamii inavyotakiwa kutumika.