Sakata la kesi ya wabunge nane na madiwani wawili waliofukuzwa waliofukuzwa na Chama cha Wananchi (CUF), limechukua sura mpya baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kugoma kutoa amri ya muda waliyoiomba wakati wa usikilizwaji wa pingamizi dhidi ya maombi yao ya zuio.
Uamuzi huo umetolewa leo, Agosti 16 na Jaji Lugano Mwandambo baada ya kusikiliza maombi ya mdomo yaliyowasilishwa na Wakili wa wadai, Peter Kibatala.
Kibatala aliomba mahakama itoe amri ya muda kwamba hali iliyopo sasa ibaki kama ilivyo kwamba wabunge wapya wasiapishwe na madiwani wasiteuliwe wala kuapishwa hadi mapingamizi ya Jamhuri yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
“Mahakama haioni tishio la chochote kutokea kati ya leo na siku ya uamuzi wa mapingamizi ya awali katika maombi ya zuio na hivyo haioni sababu ya kutoa amri za muda wakati wa usikilizaji wa mapingamizi,”amesema Jaji Mwandambo.
Kutokana na uamuzi huo wabunge hao wanasubiri Agosti 25 mwaka huu ambapo mahakama hiyo itatoa uamuzi wa mapingamizi yaliyowasilishwa na Jamhuri dhidi ya kutaka mahakama itoe zuio la kuapishwa kwa wabunge hao wapya, hadi kesi yao waliyoifungua kupinga kufukuzwa uanachama itakapotolewa uamuzi