Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Baada ya sintofahamu ya kutofikishwa mahakamani kwa viongozi sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, mahakama imesema itatoa uamuzi saa saba mchana.
Hatua hiyo imekuja baada ya mawakili wa pande zote mbili, kuingia kwa Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri anayesikiliza shauri hilo na kukubaliana nini cha kufanya.
Katika makubaliano yao mawakili hao na mahakama, wamekubaliana kuwasiliana na Magereza ili wafanye kazi yao kama hao watuhumiwa hao wanaletwa leo au hawaletwi, au mahakama iendeleea kusoma uamuzi wa dhamana hiyo.
Pande zote wamekubaliana kukutana saa saba kwa Hakimu kujua nini kimefikiwa katika makubaliano yao hayo.
Pamoja na Mbowe, viongozi wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko ambao wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwamo kuhamasisha maandamano, uchochezi na uasi.