Na ANDREW MSECHU
HALMASHAURI ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma imekuwa ya mwisho katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba yaliyotangazwa Dar es Salaam juzi.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Charles Msonde, wilaya hiyo imeshika nafasi ya 186 kati ya halmashauri 186 nchini.
Wanafunzi wa darasa la saba katika Halmashauri ya Chemba walilazimika kurudia mitihani hiyo baada ya Msonde kutangaza kuifuta kwa kile alichoeleza kuwa ni kubainika kwa kasoro hasa udanganyifu katika wilaya hiyo.
Katika matokeo hayo, halmashauri hiyo yenye shule 102 na wanafunzi 5,359 waliohitimu darasa la saba mwaka huu, imeshuka kutoka nafasi ya 176 katika matokeo ya darasa la saba ya mwaka 2017.
Matokeo hayo ni baada ya Msonde kutangaza kufutwa mitihani katika shule zote za halamashauri hiyo pamoja na baadhi ya shule katika halmashauri ya Kondoa, Kinondoni, Mwanza jiji na Ubungo kwa kosa la kuhusika kuvujisha mitihani ya darasa la saba ikiwa ni kinyume na taratibu na kanuni za mitihani nchini.
Miongoni mwa shule zilizokumbwa na kadhia hiyo ya kufutwa kwa matokeo hayo ni Shule ya Msingi Hazina na New Hazina zilizopo wilaya ya Chemba, Shule ya Msingi Kisiwani Ubungo, Shule ya Msingi Kondoa iliyopo Halmashauri ya Kondoa na Shule ya Msingi Alliance na New Alliance katika Halmashauri ya Mwanza jiji, nyingine za Alliance, New Alliance, Atlas Madale na Great Vision.
Kutokana na kufutwa mitihani hiyo, NECTA ilitangaza kurudiwa mitihani katika shule za Halmashauri ya Chemba na shule ya Hazina na Kinondoni, Anyindumina na Font of Joy za Ubungo, Alliance na New Alliance ya Mwanza jiji na Kondoa Integrity ya Kondoa mjini.
Watahiniwa katika shule hizo waliirudia mitihani Oktoba 8 na 9 mwaka huu.
Katika matokeo yaliyotangazwa jana, halmashauri nyingine zilizofanya vibaya ni
Meatu (185), Musoma Vijijini (184), Butiama (183), Lushoto (182), Mkalama (181), Uvinza (180), Rufiji (179), Kibondo (178) na Igunga (177).
Oktoba 2, Msonde akitangaza kufuta matokeo ya Chemba, alisema uchunguzi uliofanywa ulibaini baadhi ya walimu walivujisha mtihani huo wakishirikiana na waratibu elimu wa maeneo husika.
“Kuhusu shule za Halmashauri ya Chemba, uongozi wa idara ya elimu wa halmashauri hiyo ulipanga kufanya udanganyifu kupitia kwa waratibu elimu kata, walimu wakuu na wasimamizi kuhakikisha kuwa wanainua ufaulu wa halmashauri hiyo.
“Uongozi wa elimu Chemba uliunda makundi ya WhatsApp yaliyojulikana kwa jina la Elimu Chemba, Sayansi na Hisabati na wasimamizi Elimu Chemba ambayo yaliwajumuisha pia waratibu elimu kata na baadhi ya walimu wakuu, kwa lengo la kurahisisha mawasiliano baina yao.
“Katika kutekeleza azma yao, mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ulifunguliwa kabla ya wakati na kusambazwa kupitia makundi ya WhatsApp waliyokuwa wameyaunda.
“Uongozi wa idara ya elimu Halmashauri ya Chemba, ulishiriki kutoa maelekezo yaliyohakikisha maswali yanafanywa na majibu yanawafikia watahiniwa kwa wakati.
“Waratibu elimu kata walitekeleza kazi ya usambazaji wa majibu kwa walimu wakuu na watahiniwa,” alisema Dk. Msonde.
Aliwataja walioshiriki katika udanganyifu huo kuwa ni pamoja na Kaimu Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Chemba, Modest Tarimo, Ofisa Taaluma Chemba, Ally Akida, Mratibu Elimu Kata ya Farkwa, Mwalimu Noela Chambo.
Wengine ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bugenika, Joseph Mvuna, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makamaka, David Chilunda na waratibu elimu wa kata wote na walimu wakuu ambao pia walibainika kuunganishiwa kwenye makundi ya WhatsApp.