26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Halmashauri kinara wizi wa mitihani yaburuza mkia

Na ANDREW MSECHU


HALMASHAURI ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma imekuwa ya mwisho katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba yaliyotangazwa   Dar es Salaam juzi.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Charles Msonde, wilaya hiyo imeshika nafasi ya 186 kati ya halmashauri 186 nchini.

Wanafunzi wa darasa la saba katika Halmashauri ya Chemba walilazimika kurudia mitihani hiyo baada ya Msonde kutangaza kuifuta kwa kile alichoeleza kuwa ni kubainika kwa kasoro hasa udanganyifu katika wilaya hiyo.

Katika matokeo hayo, halmashauri hiyo yenye shule 102 na wanafunzi 5,359 waliohitimu darasa la saba mwaka huu, imeshuka kutoka nafasi ya 176 katika matokeo ya darasa la saba ya mwaka 2017.

Matokeo hayo ni baada ya Msonde kutangaza kufutwa  mitihani katika shule zote za halamashauri hiyo pamoja na baadhi ya shule katika halmashauri ya Kondoa, Kinondoni, Mwanza jiji na Ubungo kwa kosa la kuhusika   kuvujisha  mitihani ya darasa la saba ikiwa ni kinyume na taratibu na kanuni za mitihani nchini.

Miongoni mwa shule zilizokumbwa na kadhia hiyo ya kufutwa kwa matokeo hayo ni Shule ya Msingi Hazina na New Hazina zilizopo wilaya ya Chemba, Shule ya Msingi Kisiwani   Ubungo, Shule ya Msingi Kondoa iliyopo Halmashauri ya Kondoa  na Shule ya Msingi Alliance na New Alliance katika  Halmashauri ya Mwanza jiji, nyingine za Alliance, New Alliance, Atlas Madale na Great Vision.

Kutokana na kufutwa  mitihani hiyo, NECTA ilitangaza kurudiwa   mitihani katika shule za Halmashauri ya Chemba  na shule ya Hazina na Kinondoni, Anyindumina na Font of Joy za Ubungo, Alliance na New Alliance ya Mwanza jiji   na Kondoa Integrity ya Kondoa mjini.

Watahiniwa katika shule hizo  waliirudia mitihani Oktoba 8 na 9 mwaka huu.

 

Katika matokeo yaliyotangazwa jana, halmashauri nyingine zilizofanya vibaya ni

Meatu (185), Musoma Vijijini (184), Butiama (183), Lushoto (182), Mkalama (181), Uvinza (180), Rufiji (179), Kibondo (178) na Igunga (177).

 

Oktoba 2, Msonde akitangaza kufuta matokeo ya Chemba, alisema uchunguzi uliofanywa ulibaini  baadhi ya walimu walivujisha mtihani huo wakishirikiana na waratibu elimu wa maeneo husika.

“Kuhusu shule za Halmashauri ya Chemba, uongozi wa idara ya elimu wa halmashauri hiyo ulipanga kufanya udanganyifu kupitia kwa waratibu elimu kata, walimu wakuu na wasimamizi  kuhakikisha kuwa wanainua ufaulu wa halmashauri hiyo.

“Uongozi wa elimu Chemba uliunda makundi ya WhatsApp yaliyojulikana kwa jina la Elimu Chemba, Sayansi na Hisabati na wasimamizi Elimu Chemba ambayo yaliwajumuisha pia waratibu elimu kata na baadhi ya walimu wakuu, kwa lengo la kurahisisha mawasiliano baina yao.

“Katika kutekeleza azma yao, mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ulifunguliwa kabla ya wakati na kusambazwa kupitia makundi ya WhatsApp waliyokuwa wameyaunda.

“Uongozi wa idara ya elimu Halmashauri ya Chemba, ulishiriki kutoa maelekezo yaliyohakikisha  maswali yanafanywa na majibu yanawafikia watahiniwa kwa wakati.

“Waratibu elimu kata walitekeleza kazi ya usambazaji wa majibu kwa walimu wakuu na watahiniwa,” alisema Dk. Msonde.

Aliwataja walioshiriki katika udanganyifu huo kuwa ni pamoja na Kaimu Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Chemba, Modest Tarimo, Ofisa Taaluma Chemba, Ally Akida, Mratibu Elimu Kata ya Farkwa, Mwalimu Noela Chambo.

Wengine ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bugenika, Joseph Mvuna, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makamaka, David Chilunda na waratibu elimu wa kata wote na walimu wakuu ambao pia walibainika kuunganishiwa kwenye makundi ya WhatsApp.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles