28.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

CCM yazungumzia kutekwa Mo

ANDREW MSECHU na Aziza Masoud – dar es salaam


KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amezungumzia kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji (Mo) na kusema chama chao kimehangika sana kushughulikia tukio hilo, hivyo watu waache nongwa kwakuwa matukio ya uhalifu yanatokea duniani kote.

“Unajua watu waache nongwa, matukio haya ya uhalifu yapo duniani kote, sisi tumehangaika sana kama chama. Wametekwa watu Afrika Kusini hili si jambo la mzaha, watu wanatekwa kweli, kwa mfano Uingereza wametekwa watu miaka nane hawajarudi na polisi wanasema wanafamilia wasizungumzie hii kuonyeshwa kwamba huyo mtu hajarudi,” alisema Polepole.

Alisema kwa Tanzania kumetokea matukio mbalimbali yakiwemo ya mauaji ya watu katika wilaya za Kibiti na Mkuranga.

“Hapa kwetu tumepata shida mara kadhaa Mkuranga na Kibiti, hili jambo sisi ambao tupo katika uongozi wa chama na Serikali tunaona mzigo mzito, bahati mbaya wenzetu wanafanya mzaha kwenye mambo haya makubwa,” alisema Polepole.

Alisema kazi ya vyombo vya ulinzi na usalama ni kuhakikisha ulinzi unaimarika, hivyo inapotoea mtu ametekwa wao ndio wana kazi ya kufuatilia na kuchimbua kitaalamu kwa kushirikiana na wenzao wa kimataifa.

Polepole alisema Watanzania wamepiga maombi na dua kuhakikisha Mungu anawezesha kila chombo kinachofanya kazi kihakikishe Mo anarudi akiwa salama na kabariki ikafanikiwa, lakini cha kushangaza wapo watu wanaodai kuwa mfanyabiashara huyo hakutekwa.

“Mo amerudi anatokea mpuuzi anasema haaa, haaa Mo hakutekwa, mbona hawakumkata vidole. Sasa wakati tunaomba Mungu mlikuwa mnategemea nini? Unasema  basi ndiyo kiongozi huyo amechaguliwa na watu.

“Baadhi ya watu hao walioomba kuingia CCM wasahau tu, hatutachukua watu ambao wanashindwa kuwa na utaratibu, wanashindwa kuelewa wanatamani watu wengine wapate tabu ili waamini kweli ilikuwa tabu,” alisema Polepole.

Alisema kitendo cha Mo kurudi bila kupata madhara yoyote ni cha kumshukuru Mungu, na Serikali ya CCM wamevielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi mchana na usiku kuhakikisha wote wanaofanya vitendo hivyo wanapatikana.

“Wakipatikana washughulikiwe ipasavyo na kufanywa vitendo vyote vibaya kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wote ambao wanataka kufanya mchezo na spidi kubwa ya maendeleo ambayo tunaileta  katika taifa letu la Tanzania,” alisema Polepole.

 

BABA AZUNGUMZA

Baba yake Mo, Gullam Dewji, alisema kwa sasa mwanaye huyo afya yake inaendelea vyema.

Hata hivyo gazeti hili lilizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa mfanyabiashara huyo na kusema bado hadi jana alikuwa ajaanza kwenda ofisini.

Kuhusu waliomteka, Gullam alisema hana taarifa yoyote kuhusu kinachoendelea polisi kwa kuwa hajafuatilia.

Alisema kwa kuwa kazi hiyo iko mikononi mwa polisi, taarifa zote zitaweza kupatikana huko.

“Mimi kwa kweli sina taarifa zozote na hata sijafuatilia suala hilo. Polisi wanaweza kukueleza kwa kina kinachoendelea,” alisema.

 

WATEKAJI WASAKWA

Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema bado wanaendelea kuwasaka watu wanaodaiwa kumteka nyara Mo.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Mambosasa alisema hadi jana watu hao walikuwa bado hawajapatikana na kwamba operesheni ya kuwatafuta bado inaendelea.

“Bado hatujawapata na operesheni ya kuwatafuta inaendelea,” alisema Mambosasa alipoulizwa iwapo wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

Akizungumza baada ya kupatikana kwa Mo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro alisema hata kama watekaji hao wamemwachia Mo jeshi hilo litaendelea na operesheni yake ya kuhakikisha wanatiwa mikononi na kufikishwa mbele ya sheria.

Juzi shuhuda aliyemsaidia Mo kupata simu na kumpigia baba yake mara baada ya kutelekezwa na watekaji wake eneo la Gymkhana, alisimulia namna alivyoonana na mfanyabiashara huyo aliyekuwa amejisitiri kwa kitambaa huku akiwa kifua wazi.

Shuhuda huyo ambaye ni mlinzi katika Hoteli ya Southern Sun ya Dar es Salaam kupitia Kampuni ya Knight Support, alieleza kuwa yeye ndiye aliyempokea na kumsitiri Mo, kisha kumpa mawasiliano yaliyomuunganisha na baba yake.

Alisema Mo baada ya kutelekezwa na watekaji, alifika hotelini hapo akiongozana na mlinzi mmoja wa jirani na alipotelekezwa.

Kwamba alipomuona Mo hakuweza kumtambua hadi alipojitambulisha, kutokana na namna alivyoonekana ambapo alikuwa amejifunga kipande cha kitambaa kinachoonekana kama vitambaa vinavyotumika kuweka matangazo barabarani.

“Kwa namna alivyokuwa amevaa, yeyote kwa haraka asingemtambua, kiunoni alikuwa amejifunga kitambaa kinachoonekana kama vile vya matangazo, akiwa amekivaa kama msuli, juu akiwa kifua wazi,” alisema.

Mo alitekwa nyara na watu wasiojulikana alipowasili kwenye kituo cha mazoezi cha Hoteli ya Colloseum jijini Dar es Salaam saa 11 alfajiri ya Oktoba 11, mwaka huu kisha kutelekezwa katika eneo la viwanja vya Gymkhana usiku wa kuamkia Oktoba 20, ikiwa ni siku tisa tangu kutekwa kwake.

Watekaji hao walimwacha katika eneo hilo la Gymkhana na kutelekeza gari inayodaiwa kuwa ndiyo iliyotumika kumteka nyara kisha kutokomea kusikojulikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,085FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles