Asha Bani
Taasisi isiyo ya Serikali ya HakiElimu wametoa angalizo kwa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia katika bajeti ya mwaka huu huku wakiitaka itengwe fedha za kutoshana kufanya utekelezaji wa mipango yake kama ambavyo ilivyopangwa.
Changamoto hizo ni pamoja na utekelezwaji wa bajeti katika kuongeza bajeti ya sekta ya elimu, bajeti kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika elimu ya msingi na bajeti ya maendeleo ya elimu ya msingi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mkurugenzi Mtendaji, HakiElimu Dk John Kalage amesema licha ya serikali kufanikiwa katika ongezeko la udahili wa idadi ya wanafunzi wa shule ya msingi kwa asilimia 17 lakini mazingira yake bado hayaridhishi.
Dk John amesema udahili umeongezeka kwa asilimia 17 kutoka wanafunzi 8,639,202 mwaka 2016 hadi kufikia wanafunzi 10,111,255 kwa mwaka 2018.
Pia amesema changamoto nyingine ambayo serikali inatakiwa kuiangalia kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ni la upungufu wa madarasa kwa shule za msingi kwa asilimia 85, mashimo choo 83, nyumba za walimu 66 na asilimia 14 madawati.
Kwa shule za sekondari upungufu asilimia 52 vyumba vya madarasa, asilimia 84 maabara, asilimia 86 madawati ,asilimia 85 nyumba za walimu, asilimia 88 mabweni ya wanafunzi na asilimia 53 mashimo ya choo.
Kutokana na hali hiyo wameitaka bajeti ya fedha ya mwaka huu kutenga hela za kutoshana kufanya utekelezaji wake kama ambavyo imepangiwa.