Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
MWILI wa gwiji wa habari nchini, Chrysostom Rweyemamu maarufu ‘Mwalimu’ (64), unatarajiwa kuagwa leo nyumbani kwake Mbweni Dar es Salaam.
Rweyemamu alifariki dunia Jumamosi saa 2:30 usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa mujibu wa maelezo ya daktari kwa watoto na mke wake ambao walijulishwa taarifa za kifo hicho juzi alfajiri walipokwenda kumjulia hali.
Ratiba iliyotolewa na familia jana ilieleza kuwa shughuli za kumuaga zitaanza saa 4.00 asubuhi nyumbani kwake ambako viongozi na wanahabari mbalimbali wanatarajiwa kushiriki.
Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Dimba na The African, Absalom Kibanda, alisema jana kuwa shughuli hiyo itafanyika saa 4 hadi 5 asubuhi kwa kuwa na ibada fupi nyumba kwa marehemu Mbweni kwa Masanja.
“Baada ya ibada fupi mwili wa marehemu utapelekwa Kanisa Katoliki Mbweni ambako baada ya ibada itakayoanza saa 5 hadi 6, mwili utasafirishwa kwend wilayani Muleba mkoani Kagera kwa mazishi yatakayofanyika keshokutwa,” alisema Kibanda
Alisema Rweyemamu alikuwa akisumbuliwa na uvimbe tumboni kwa kama wiki tatu hivi kabla ya kulazwa Ijumaa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alifanyiwa upasuaji, kabla ya hali yake kubadilika baadaye na akafariki dunia Jumamosi usiku.
Akizungumzia msiba wa baba yake, mtoto mkubwa wa marehemu, George Chrysostom alisema kilikuwa kifo cha ghafla kwa sababu hadi wanaondoka Muhimbili Jumamosi jioni hali ya baba yakr ilikuwa ikiendelea vema.
Alisema baba yake alikuwa akizungumza vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe tumboni.
“Baba alikuwa mzima na alikuwa akizungumza na hata kuwatambua watu wote waliokuwapo pale na aliweza kwenda kuoga vizuri jioni ya jana (juzi) kabla ya wao kuondoka,” alisema George.
Alisema kwa mujibu wa maelezo waliyopewa na daktari aliyekuwa akimtibu, baba yake kabla ya kufikiwa na mauti alianza kupata shida ya kupumua ghafla hatua iliyosababisha daktari aliyekuwa akimhudumia kuitwa kujaribu kuokoa maisha yake lakini haikuwezekana.
Alisema daktari aliwaeleza kwamba upo uwezekano mkubwa kwamba marehemu alipata tatizo la damu kuganda katika mapafu hali iliyosababisha apate mshituko wa moyo uliochukua maisha yake.
Mtoto huyo wa marehemu alisema mwili wa baba yake unatarajiwa kusafirishwa leo kwenda kwao, Kishanda katika Kijiji cha Iyunga Wilaya ya Muleba mkoani Kagera ambako mazishi yatafanyika keshokutwa.
Mwalimu Chrysostom Rweyemamu ameacha mjane na watoto watatu wa kiume.
Marehemu Chrysostom Rweyemamu, alijiunga na Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Oktoba mwaka 1999 wakati huo ikijulikana kama Habari Corporation na kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Maarifa Media Trust. (MAMET)
Jana wanahabari mbalimbali wakongwe waliowahi kufanya kazi na marehemu Chrysostom, walikuwapo nyumbani kwake, wakiwamo Jenerali Ulimwengu, Dk. Gideon Shoo, John Bwire na Mayage S. Mayage.
Kabla ya kukutwa na umauti, Jumamosi ya wiki iliyopita marehemu alifanyiwa upasuaji wa uvimbe siku ya Ijumaa na hali na alitoka vizuri katika upasuaji huo na kuamka salama lakini hali yake ilibadilika baadaye.
Mwakyembe amlilia
Waziri wa Habari,, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema amepokea kwa mshtuko kifo cha mwanahabari Chrysostom Rweyemamu kwa sababu anamfahamu gwiji huyo wa habari kutokana na uhodari wake katika masuala ya habari.
“Ninapenda kutoa salamu zangu za pole kwa Kampuni ya magazeti ya New Habari (2206) Ltd, familia, ndugu, jamaa na marafiki na wana tasnia ya habari na watanzania wote nchini. Ninawaomba muwe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na gwiji huyu wa habari,” alisema Dk. Mwakyembe katika taarifa yake.
Hadi mauti yanampata marehemu Chrysostom, alikuwa Mhariri wa Mafunzo wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd.