26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

GWAJIMA: KAZI NDIYO IMEANZA

Na Aziza Masoud – Dar es Salaam

ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ameachiwa huru pasipo masharti yoyote na Jeshi la Polisi Dar es Salaam lililokuwa likimshikilia kwa tuhuma za dawa za kulevya na kuielezea hatua hiyo kuwa ni mwanzo wa safari nyingine mpya.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili muda mfupi baada ya kuachiwa jana saa 11:00 jioni, Askofu Gwajima alisema jambo la kwanza atakalolifanya ni kurudi polisi kesho kuchukua vitu vyake na kumtembelea mfanyabiashara maarufu, Yusuph Manji ambaye waliwekwa pamoja katika chumba maalumu.

Askofu Gwajima ambaye alikuwa akishikiliwa na polisi tangu  Alhamisi ya wiki hii, alipokwenda  kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye alimtaja katika orodha ya majina 65 ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya, alisema ni mapema mno kuzungumzia hatua ambazo atazichukua baada ya kuachiwa.

Wakati akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana saa 12:00 jioni, Askofu Gwajima ambaye alikuwa akielekea sehemu maalumu kwa mapumziko, alisema ataliachia kanisa liamue.

“Hii vita ndiyo kwanza imeanza, kwa sasa zimeanza kukunjwa ngumi, kuhusu mimi kuchukua hatua za kisheria siwezi sema kwa sasa kwa sababu mimi ni kiongozi wa kidini, kanisa litakaa na kuangalia nini kitafuata,” alisema Askofu Gwajima.

Akisumulia yaliyotokea baada ya kuripoti Polisi Alhamisi wiki hii, Askofu Gwajima alisema alihojiwa na kupekuliwa nyumbani kwake na baadae alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kuchukuliwa vipimo vya mkojo na damu.

 Alisema katika vipimo hivyo ambavyo nakala zake anazo, hawakukuta viashira vyovyote vinavyoonyesha kuwa anatumia dawa za kulevya.

“Walinipeleka kwa mkemia mkuu wakachukua vipimo vya ‘urine’ (mkojo) na damu, wakapima vyote wakakuta hamna kitu na nakala zangu zote ninazo,” alisema Askofu Gwajima.

Alisema chumba alichokuwa akiishi mahabusu kwa kipindi cha siku tatu, kilikuwa kimetengwa maalumu na alikuwa pamoja na Manji.

Alipoulizwa kama Makonda aliwahi kuonana naye wakati alipokuwa mahabusu, alijibu kuwa hakuwahi kuonana na mkuu huyo wa mkoa hadi alipopatiwa dhamana na kuondoka kituoni hapo.

“Sikuonana na Makonda, labda kama alikuwa akija pale kituoni anaingia kuwaona watu wengine, kwa sisi hatukumuona, mimi na Manji tulikuwa chumba kimoja, hatukumuona kabisa,” alisema Askofu Gwajima.

Awali baada ya Askofu Gwajima kuachiwa huru, nje ya kituo cha polisi walionekana baadhi ya  waumini wake wakishangilia huku wakitoa maneno mbalimbali ya furaha.

Askofu Gwajima ambaye alikuwa ameongozana na watu watano akitokea kituoni hapo, alipokewa na waumini kwa shangwe na vigelegele.

Mmoja wa waumini alisikika akisema ‘tumeshinda’ na mwingine alisikika akisema  ‘hongeraa baba, tumeshinda baba’.

Waumini hao ambao walikuwa wakimsindikiza kuelekea sehemu ambako gari lake lilikuwa limeegeshwa, mbali na kuonyesha furaha waliyonayo kwa maongezi, pia walionekana wakichukua picha kupitia simu zao za mkononi.

MTANZANIA Jumapili lilipowasiliana na msemaji wa askofu huyo, Esther Wasira ili kujua ratiba yake kwa siku ya jana, alisema kwa sasa wanafahamu kwamba amepumzika .

“Sisi tupo kanisani tunasherehekea, lakini yeye hayupo, kawekwa mahali amepumzika, hata mimi alipo sipafahamu,” alisema Esther.

Taarifa za kuachiwa kwa Askofu Gwajima zilianza kusambaa kupitia ukurasa wake  wa instagram  ambao uliandikwa ujumbe uliosomekana “FREE AT LAST: Mungu awabariki wote mlioomba kwa ajili ya jambo hili”.

Ujumbe huo ambao uliashiria kuachiwa huru kwa kiongozi huyo wa kiroho, ulizua taharuki kubwa na kusababisha baadhi ya watu kusambaza taarifa kuwa ameachiwa.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro kwa simu ili aweze kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, aliikata simu baada tu ya mwandishi kujitambulisha.

Mbali na Askofu Gwajima, katika sakata hilo la dawa za kulevya, Makonda pia aliwataja wafanyabiashara, wanasiasa na wasanii ambao baadhi yao bado wanashikiliwa na polisi.

Watuhumiwa hao kwa pamoja hatma yao ya kufikishwa mahakamani ama kuachiwa huru itajulikana kesho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles