27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

MAKONDA ABADILI STAILI

Na MWANDISHI WETU – dar es salaam

TANGU Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda atangaze orodha mpya ya watu 65 iliyojumuisha wanasiasa na watu wengine maarufu Jumatano wiki hii, na kuwataka wafike Kituo Kikuu cha Polisi wakajadiliane juu ya tuhuma za dawa za kulevya, kiongozi huyo hajaonekana tena hadharani.

Tofauti na wiki iliyopita wakati alipotangaza kwa mara ya kwanza orodha ya watuhumiwa wa dawa za kulevya iliyowajumuisha askari polisi 17, wasanii na watu mbalimbali 18, Makonda alikuwa akionekana polisi kwa uwazi na hata kuelezwa kushiriki mahojiano na watuhumiwa hao.

MTANZANIA Jumapili limebaini kuwa tangu atangaze awamu ya pili ya watuhumiwa hao 65, Makonda hajaonekana na wala hajakutana na watuhumiwa hao.

Si hilo tu, pia hajafanya mikutano na waandishi wa habari kueleza nani kafika na nani hajafika miongoni mwa watuhumiwa hao.

Taarifa hizi zinathibitishwa pia na Askofu wa Kanisa na Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambaye muda mfupi baada ya kuachiwa jana jioni, aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa hajawahi kukutana wala kuonana na Makonda katika mahojiano kituoni hapo tangu aliporipoti Alhamisi wiki hii.

Mara baada ya kutangaza orodha ya kwanza, Makonda alifika mara kadhaa kituoni hapo na hata kufanya mkutano na waandishi wa habari akiwa ameambatana na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro.

Katika mkutano huo ambao Makonda aliutumia kueleza matarajio yao ya kuwafikia wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya, pia aliwataja watuhumiwa walioripoti na ambao hawakuripoti.

Zaidi aliutumia mkutano huo kuwaongeza kwenye orodha ya watuhumiwa wa dawa za kulevya, mwanamuziki Vanessa Mdee, mrembo anayependezesha video za muziki, Tunda na askari wengine watano ambao nao aliwataka wafike kuripoti kituoni hapo Jumatatu ya wiki iliyopita.

Ingawa zipo taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba Makonda alifika kituoni hapo juzi, lakini alifanya hivyo kimya kimya.

Juzi ikiwa siku moja baada ya watuhumiwa wawili kuripoti kituoni hapo na kuwekwa ndani, Kamanda Sirro alifanya mkutano na waandishi wa habari chini ya mti uliopo nje ya kituo hicho cha polisi pasipo uwepo wa Makonda.

Sirro aliitaja orodha ya watu waliofika hadi kufikia juzi kuwa ni wanne tu kati ya 65 waliokuwa wametajwa na Makonda.

Jana ikiwa ni siku tatu tangu Makonda atangaze orodha hiyo ya awamu ya pili, lakini pia Jeshi la Polisi likimwachia Askofu Gwajima, bado kiongozi huyo alibaki kimya zaidi ya kutuma picha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, ikimwonyesha akiwa nyumbani kwake na mwanamuziki wa Bongo Fleva, Khalid Mohamed ‘TID’.

TID ni miongoni mwa wasanii na watu mbalimbali 18 ambao Makonda aliwatangaza kwenye sakata la dawa za kulevya katika orodha ya kwanza wiki iliyopita.

Msanii huyo ni miongoni mwa wale ambao walifikishwa mahakamani mwanzoni mwa wiki hii kutokana na kosa la kujihusisha na dawa za kulevya.

“Mungu wetu hajalala na siku zote anampenda amtafutae, karibu tena nyumbani TID.” aliandika Makonda katika mtandao wake wa Instagram.

Picha kama hiyo pia aliiweka TID katika ukurasa wake wa Instagram ikiwa imebeba maandishi yanayosomeka: “Muziki bila madawa ya kulevya inawezekana… This is the turning Point kwangu mimi na kizazi cha mziki huu wa kizazi kipya, nikiwa na Mh. Makonda leo tukijadili Jinsi gani ya kuokoa vipaji na sanaa kwa ujumla, Mungu ibariki Bongo Fleva, Mungu Ibariki Tanzania”.

Mara kadhaa MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Makonda ofisini kwake na kupitia simu ya mkononi bila mafanikio.

Tangu aibuke wiki iliyopita na operesheni ya kupambana na dawa za kulevya katika mkoa wake wa Dar es Salaam, Makonda ametaja orodha mbili tofauti za watuhumiwa wa dawa hizo.

Wakati akitangaza orodha ya pili, Makonda alisisitiza kuwa habahatishi na kwamba watu aliowataja tayari wamefanya uchunguzi wa kutosha dhidi yao.

Kampeni hiyo ilionekana kugusa moja kwa moja mamlaka za juu baada ya hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli wakati akimwapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, kutumia fursa hiyo kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuingia katika vita hiyo na kuhakikisha kila anayehusika anakamatwa bila kujali umaarufu wake.

Kabla ya kauli hiyo ya Rais Magufuli, operesheni hiyo aliyoianzisha Makonda ilionekana pia kuigusa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Katika hatua ambayo pengine haikutarajiwa na wengi, ikiwa ni siku tatu tu tangu Makonda aanze operesheni yake, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu alitangaza kuwasimimamisha kazi askari 12 ambao majina yao yalitajwa kwenye orodha ya  Makonda Alhamisi na Ijumaa ya wiki iliyopita.

Hata hivyo, upepo ulionekana kuvuma vibaya upande wa Makonda baada ya suala hilo kufika bungeni ambako baadhi ya wabunge walimpinga vikali kwa hoja kwamba operesheni yake hiyo ilikuwa haijazingatia misingi ya kisheria.

Wakati Bunge likiwa na mtazamo huo, baadhi ya watu wanaomuunga mkono walikuwa na hoja kwamba Makonda ndiye mtu pekee aliyethubutu kuwataja kwa majina watuhumiwa tofauti na viongozi wengine waliopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles