NA RAS INNO,
UCHAGUZI wa Taifa dogo la Afrika Magharibi la Gambia lililopo kilometa chache ukingoni mwa Jangwa la Sahara, uligubikwa na mvuto wa kipekee kutokana na wasifu wa wagombea wawili waliochuana vikali. Rais aliyebwagwa katika uchaguzi huo, Yahya Jammeh, aliyetawala kwa miongo miwili na ushei aliyeingia madarakani kwa Mapinduzi ya kijeshi amekubali kushindwa na kuahidi kukabidhi madaraka kwa amani kwa mpinzani wake aliyeshinda, Adama Barrow, ambaye hajawahi kuongoza katika ngazi yoyote ya kisiasa.
Wagombea wote wawili wanawiana kwa umri (miaka 51) ambapo Jammeh aliyeingia madarakani kwa Mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu mwaka 1994 alijipatia asilimia 36 ya kura zote zilizopigwa, Barrow alijipatia asilimia 45 na mgombea wa tatu Kandeh alijipatia asilimia 17.8. Pengine matokeo hayo yaliyopokewa kwa nderemo na vifijo si kivutio kikubwa zaidi cha uchaguzi, lakini ni mfumo mbadala wa Taifa hilo katika kupiga kura unaotofautiana na mataifa mengine kwa kutotumia kadi za kupiga kura bali kinachotumika ni gololi zisizokuwa na rangi wanazotumbukiza wapiga kura katika pipa lenye rangi inayomwakilisha mgombea wanayetaka kumchagua.
Kuanguka kwa gololi hiyo ndani ya kitako cha pipa na kutoa sauti ya kugonga humwezesha msimamizi wa uchaguzi kutambua endapo mpiga kura yeyote atajaribu kupiga kura zaidi ya moja anayopaswa kutumbukiza. Ni mfumo ulioanza kutumika mwaka ambao wagombea Jammeh na Barrow walizaliwa (1965), kutokana na kiwango duni cha elimu miongoni mwa Wagambia wengi ambao wasingeweza kutumia mfumo uliozoeleka unaohusisha kuandika.
Kutokana na upande wa chini kwa ndani ya pipa kutoa sauti inayorandana na kengele ya baiskeli siku ya kupiga kura hairuhusiwi kuja na baiskeli katika kituo cha kupiga kura ili kutosababisha mkanganyiko. Mapipa hayo huwekwa sanjari ili isiwezekane kuinua mojawapo na kubaini matokeo kabla ya kuhesabiwa kutokana na uzito kwa wingi wa gololi, kila pipa hupakwa rangi ya chama cha mgombea na kuwekwa jina la chama anachowakilisha na picha ya mgombea.
Baada ya kupiga kura mpiga kura huchovya kidole katika wino kuthibitisha kuwa ameshiriki katika kupiga kura. Katika kuhesabu kura gololi hizo huwekwa kwenye ubao wenye vishimo kati ya 200 hadi 500 ili kurahisisha kazi ya kuhesabu. Mshindi wa uchaguzi huo, Barrow, aliyezaliwa katika kijiji kidogo Mashariki mwa Mji wa Basse alihamia jijini London mwaka 2000 kutafuta maisha kwa kufanya kazi ya ulinzi wa duka la bidhaa huku akisomea uwakala wa Mthamini Majengo na baada ya kuhitimu alirudi Gambia na kufungua kampuni yake anayoiendesha hadi sasa.
Barrow aliyeongoza muungano mkubwa zaidi kuwahi kuundwa tangu Taifa hilo lijipatie uhuru wa vyama saba vilivyomsimamisha kuwa mgombea, katika kampeni aliahidi kuboresha uchumi wa Taifa hilo uliodorora na kusababisha mamia ya Wagambia kufunga safari za hatari ili kuingia Ulaya wakiwa wahamiaji haramu. Mojawapo ya vipaumbele alivyoahidi kushughulikia ni pamoja na kuunda Serikali ya mpito ya miaka mitatu, itakayojumuisha watendaji kutoka muungano wa vyama vilivyomsimika katika kuelekea kuweka muhula wa vipindi viwili vya ukomo wa utawala uliokosekana na kusababisha Rais Jammeh aliyeshindwa kutawala kwa miaka 22.
Licha ya Barrow kuongoza muungano mkubwa wa vyama katika uchaguzi haikutarajiwa kwa matokeo yaliyojiri hususani kwa Rais Jammeh kukubali kushindwa, kwa kuwa miezi michache kabla ya uchaguzi wapinzani walisukwasukwa na kukataliwa kwa waangalizi wa Kimataifa pia kuzimwa mitandao ya kijamii siku ya uchaguzi. Ni wimbi jipya linalotokea ukanda wa Afrika Magharibi kwa viongozi walioko madarakani kukubali matokeo wanaposhindwa kwenye uchaguzi kama ilivyotokea nchini Nigeria kwa Rais Goodluck Jonathan kukubali kushindwa na Muhammadu Buhari.
Yahya Jammeh mhafidhina wa imani ya Kiislamu aliwahi kutamka kuwa atatawala hata kwa miaka bilioni moja kama ‘Allah’ akipenda, lakini kitendo chake cha kukubali kushindwa kimeamsha shangwe za kutoamini kwa kuwa aliitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma na kuwasweka kifungoni baadhi ya wapinzani walioonesha kupinga utawala wake.
Kuna nyakati alijihusisha na fani tatanishi ya tiba mbadala alipodai kuwa amegundua tiba ya Ukimwi na ugumba kwa njia ya miujiza. Inavyoelekea Allah aliyemtegemea Jammeh ameamua kuleta mabadiliko ya mustakabali wa Taifa hilo lililokuwa linaelekea kujitenga na dunia, kutokana na Rais Jammeh kudhamiria kuiondoa Gambia katika uanachama wa Jumuiya ya Madola na Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC), mambo ambayo Rais Mteule Barrow ameahidi kuyatengua. Inawezekana Allah pia amembadilisha Jammeh kwa kuwa katika kukubali kwake kushindwa alimpigia simu Barrow na kumwambia: “Hongera, mimi ni Rais ninayetoka madarakani, wewe ni Rais unayeingia madarakani, nchi itakuwa mikononi mwako kuanzia Januari, nakuhakikishia kukupa ushirikiano utakaouhitaji!”
Baadaye katika hotuba yake kwa Taifa kwa njia ya luninga, Jammeh alitamka kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa wazi zaidi kutokea duniani kote na anachukua fursa hiyo kumpongeza Barrow kwa ushindi dhahiri, akimtakia mema yeye na Wagambia wote kwamba akiwa Mwislamu safi hatahoji uamuzi wa Allah aliyeamua kupitia Wagambia. Hakika, hatimaye gololi zimeamua mustakabali wa nchi ya Gambia!