24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

HATUA AMBAZO CHINA ITACHUKUA DHIDI YA ‘UCHOKOZI’ WA TRUMP

Republican U.S. presidential nominee Trump speaks as Democratic U.S. presidential nominee Clinton listens during their presidential town hall debate in St. Louis
Donald Trump. picha ndogo ni Rais wa Taiwan, Tsai Ing-wen

JOSEPH HIZA Na Mashirika ya Habari

WACHINA waliamka Jumatatu ya wiki hii wakikutana na mashambulizi makali kutoka kwa Rais Mteule wa Marekani Donald Trump, siku chache tu baada ya  kukasirishwa na kitendo chake cha kuwasiliana na Rais wa Taiwan, Tsai Ing-wen.

Wakati wasaidizi wa Trump wakijaribu kumtetea bosi wao huyo kuwa alipokea simu hiyo akiwa hana hili wala lile, maofisa wa Taiwan wanasema ni zoezi la kimkakati lililopangiliwa vyema.

Kitendo hicho kilifanya Marekani ivunje itifaki ya miongo kadhaa inayozuia viongozi wake kuwasiliana moja kwa moja na wale wa Taiwan, kwa vile China inasisitiza kisiwa hicho ni mali yake.

Mpango huo haukuihusisha Wizara ya sasa ya Mambo ya Nje kama anavyosema Waziri John Kerry.

Tukio hilo na mengine linaonesha namna utawala wa Trump utakavyokuja na mpya linapokuja suala la sera za kigeni.

Namna hii Trump anavyoshughulikia mambo ya kigeni imewatia wasiwasi wataalamu wa Serikali wakiwamo wa intelijensia, ambao wanalalamika namna anavyopuuza taarifa za siri za kiusalama, wanazompatia.

Kama hayo hayatoshi, Trump alilikoroga zaidi kwa kuituhumu China kupitia mtandao wa Twitter kuwa imekuwa ikishusha thamani ya sarafu yake kwa malengo ya kuuza zaidi bidhaa zake, kitu ambacho ni kinyume na inavyotokea na pia ameituhumu kujenga kambi ya jeshi katika Bahari ya China Kusini, kitu ambacho ni kweli.

Na hivyo mawasiliano ya simu na Tsai kunaweza kuwa mwanzo wa mhamo wa sera iliyozoeleka na kuja na yake mwenyewe inayoonekana kuipeleka Marekani kule, ambako wadadisi wa mambo wameshindwa kubaini bado.

Lakini wanaharakati wa haki za binadamu duniani na wahafidhina ndani ya chama cha Republicans, anachotokea Trump wamekuwa wakiiponda sera ya muda mrefu ya Marekani kuichukulia Beijing ‘bora liende’ kuwa haijawaletea matokeo inayotaka.

Lakini pia hatari ya kubadili mwelekeo sera dhidi ya China ni kuwa hakuna ajuaye namna taifa hilo kubwa la Asia linaloongozwa na Rais anayechukuliwa kutokuwa na ‘Msalie mtume’ dhidi ya maadui wake wa kisiasa, litakavyoitikia.

Hata hivyo, hizi ni hatua ambazo China inaweza kuchukua kutokana na mzozo huo;

Kupuuza. Wizara ya Mambo ya Nje ya China tayari imesema Trump aliingizwa ‘mkenge’ na Taiwan kwa kujikuta hana jinsi zaidi ya kupokea simu kutoka kwa Rais Tsai Ing-wen.

Kwa mwelekeo huo, Beijing inaweza kulichukulia suala hili kirahisi na kupuuza kana kwamba hakuna kilichotokea, pamoja na ukweli kuwa Trump alikusudia kama tulivyowasikia maofisa wa Taiwan.

Hatua kama hizi za kuchukulia mambo kirahisi si mpya kwa China, iliwahi kufanya hivyo wakati Marekani ilipotuma manowari za kivita katika eneo la mgogoro la Bahari ya Kusini China, ambalo Beijing inadai ni lake.

China badala ya kutumia nguvu nyingi kulishughulikia, iliionya tu Marekani kuwa vitendo kama hivyo vya kichokozi vinaweza kuwaingiza vitani huko mbele.

Kwa vile Trump hajaingia bado madarakani, kunaipa Beijing uamuzi rahisi wa kupuuza kilichotokea licha ya kuwa nyendo za bilionea huyo dhidi ya China, zinaweza kuifanya Serikali ya Xi Jinping ionekane dhaifu nyumbani.

Adhabu kwa Serikali ya Taiwan. Kwa vile bado Trump hajawa rasmi Rais, China haiwezi kumlenga, lakini inaweza kuiadhibu Taiwan kama ujumbe wa onyo kwa Trump, hili lilielezwa na gazeti la kizalendo nchini humo, Global Times.

Miongoni mwa njia ni kushinikiza mataifa machache ikiwamo Vatican City na Panama, ambayo yana uhusiano wa kidiplomasia na Taiwan yaachane na kisiwa hicho.

Adhabu kwa biashara za Taiwan. Itakuwa rahisi kwa Beijing kuwekea vikwazo bidhaa za Taiwan kuliko kuanza vita za kibiashara na Marekani, wadadisi wa mambo wanaamini.

Kwa sababu China ni mshirika mkubwa wa Taiwan kibiashara, mabadiliko yoyote ya biashara yanaweza kuwa pigo kubwa kwa kisiwa hicho.  Taiwan imeuza bidhaa za kielektroniki zenye thamani ya Dola bilioni 29 kwa China mwaka 2015, ikiwa ni mauzo makubwa zaidi ya kigeni.

Hilo ndilo linalowezekana kuliko vikwazo vya biashara dhidi ya Marekani, kwa sababu China na Marekani kwa pamoja zinategemeana mno kiuchumi, wachambuzi wa mambo wa mataifa haya wanakubaliana.

Kwa kuhofia hilo, tayari wafanyabiashara wa Taiwan wameonesha hofu kwa mwasiliano ya simu baina ya Trump na Tsai na wamejitokeza kuiunga mkono China

Himaya ya migahawa maarufu ya vyakula vya baharini wa Hai Pa Wang nchini Taiwan ulinunua tangazo la biashara gazetini ukiahidi kuunga mkono ‘China moja’ huku Serikali ya Taiwan ikilaani China kuingiza siasa katika sekta ya biashara ya Taiwan.

Ahabu kwa kampuni za Marekani. Baadhi ya kampuni kubwa za Marekani na zinazotengeneza ajira nyingi hutegemea kwa kiasi kikubwa soko la China. Hizo ni pamoja na Apple, Boeing na General Motors kwa kutaja chache.

Tayari gazeti moja linaloungwa mkono na Serikali limeshaonya kuwa China itaacha kununua ndege za Boeing, bidhaa za elektroniki za iPhones  na bidhaa za kilimo za Marekani iwapo Trump ataonesha utoto ikiwamo kuweka kodi kubwa dhidi ya bidhaa za China kama alivyoahidi mara kadhaa.

Kampuni za teknolojia za Marekani tayari zimeonesha wasiwasi na zimeshakumbana na vikwazo vyenye lengo la kufanya iwe ngumu zaidi kufanya biashara China.

Wafanyabiashara wa Marekani wamezuiwa kuwekeza katika sekta fulani na wanapata ugumu wa kuondoa fedha zao kutoka China. Na hivyo vikwazo vyovyote au sheria kali zaidi zitawadidimiza  moja kwa moja.

Hata hivyo, njia nyingi zinaweza kuiumiza zaidi China kuliko Marekani,” anasema profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Peking nchini China.

Vita yoyote ya kibiashara itawasumbua wauzaji wa China katika uchumi dhaifu kuliko Marekani,” alisema akikumbushia kwamba kampuni za Marekani zinatengeneza bidhaa kwa ajili ya China nchini China ni nyingi kuliko zile  za China zinazotengeneza kwa ajili ya Marekani nchini Marekani.

Kusitisha uhusiano na Marekani. Wakati wazo la mataifa haya makubwa zaidi kiuchumi duniani kuacha kuwasiliana, likionekana gumu kutokea, baadhi ya wadadisi wa kisiasa wa China wanalipendekeza.

“Iwapo ataendelea kuihesabu Taiwan nchi, tunapaswa kuvunja naye uhusiano,” Shen Dingli, Professa wa uhusiano wa kimataifa wa Chuo Kikuu cha Fudan, Shanghai anasema.

“Sifahamu nini Serikal itakachofanya, lakini najua iwapo ni mimi nitavunja uhusiano wetu.”

Kwa vile Marekani iliitambua Serikali moja ya Beijing mwaka 1979, haijawahi kutokea kwa mataifa haya kususiana moja kwa moja ijapokuwa Marekani iliondoa ubalozi wakati Serikali iliposhughulikia kikatili waandamanaji katika kiwanja cha Tiananmen mwaka 1989.

Kuitishia Taiwan kijeshi. Hili likitokea China itavuka mipaka, maana daima husema itashughulikia suala la Taiwan kwa njia za amani ikiwamo pale itakapodai uhuru.

Baada ya Marekani kutoa viza kwa kiongozi wa Taiwan, Lee Teng-hui mwaka 1995, Beijing ililipiza kisasi kwa kufanya mazoezi ya kijeshi karibu na Taiwan ikiwamo kufanya majaribio ya makombora.

Kuitisha Marekani kijeshi. Kuna uwezekano wa kuibuka mgogoro baina ya China na Marekani huko mbele kuhusiana na suala la Taiwan.

China ina jeshi kubwa zaidi duniani lenye askari milioni 2.3 kulinganisha na Marekani yenye askari milioni 1.5 na ina vifaa vya kisasa mbali ya mamia ya meli.

Kitu ambacho Trump na washauri wake huenda hawakijui ni kuwa Serikali ya China inaichukulia Marekani kama tishio kubwa kwake kijeshi.

Sababu ya kutokuwapo hali ya wasiwasi baina yao ni kutokana na Marekani kuwa mwangalifu isiikasirishe China kwa miaka mingi na hivyo kutokuwapo na migongamano mikubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles