Na Mwandishi Wetu, Mwanza
ILI kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa kwa wanafunzi wa kike na kiume kuanzia elimu ya msingi mpaka chuo, Shirika la Wanawake Waelimishaji Afrika (Fawe) tawi la Tanzania limewajengea uwezo walimu tarajali katika mbinu za ufundishaji na ujifunzaji zinazozingatia usawa wa kijinsia.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamefunguliwa leo Juni 25, 2024 katika Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza hadi Juni 27, mwaka huu, huku elimu hiyo ikitarajia kuwapa mbinu za ufundishaji unaokidhi mahitaji maalum ya kielimu kwa wasichana na wavulana.
Mkurugenzi wa Fawe Tanzania, Neema Kitundu, amesema elimu wanayoitoa itasaidia kuvunja ukimya na upendeleo ambao umezoeleka kutokana na mila, desturi na mapokeo yaliyopo kwenye jamii kwamba mtoto wa kike anapaswa kukaa kimya, jambo ambalo linamzuia kushiriki kikamilifu katika suala zima la ujifunzaji.
“Kama mwalimu hana hizi mbinu na maarifa ya kufundisha kwa kuzingatia usawa wa kijinsia atawaacha nyuma wasichana. Tunaona kwamba haya mafunzo yataleta tija na maendeleo kwa sababu wakimaliza chuo watakuwa nayo kichwani atatoka ameiva na kuitumia katika ufundishaji,” amesema Kitundu.
“Tunawapa maarifa walimu ni kwa namna gani watawasaidia wanafunzi hata kama wanafanyiwa ukatili ni namna gani wawakomboe, kuwasaidia ili waondokane na ukatili huo. Pia tunawaonyesha madhara ya ukatili, kujiheshimu, kujitambua na kujithamini ili wasikumbane na vitendo hivi,” amesema
Mwenyekiti wa wanufaika wa afua za Fawe Tanzania, Cheka Omari, amesema afua za zinazotekelezwa na shirika hilo zinawajengea uwezo wanafunzi wa kike na wa kiume kujitambua, kujiamini, kujiheshimu na kujithamini, hivyo, kuwa na uwezo wa kubaini changamoto zinazomzunguka na kupata suluhisho la kuzitatua.
“Tunataka tuwaambie wadogo zetu ambao wako shuleni kwamba changamoto haziishi na zipo kila kona, jambo la msingi ni wao kuona kwamba anakabiliwa na changamoto ipi na ataitatuaje,” amesema Cheka
Kwa upande wake, Mkuza Mitaala Taasisi ya Elimu Tanzania, Given Mbakilwa, amesema suala la usawa wa kijinsia limezingatiwa katika maboresho ya mtaala wa mwaka 2023 kuanzia elimu ya msingi hadi chuo ili wanafunzi waanze kutambua vitendo hivyo katika hatua ya awali na kujua haki zao.
“Tumegundua watoto wengi wanafanyiwa ukatili wa kijinsia lakini wanaogopa kutoa taarifa kwa sababu pengine aliyefanya ni mwalimu anayeogopeka kwahiyo anahofia hatima yake. Kwahiyo kupitia elimu hii walimu wanaojifunza ualimu tayari wamechopekewa umahili wa kutambua ukatili wa kijinsia na kuupiga vita,” amesema Mbakilwa
Mmoja wa walimu tarajari wa chuo hicho aliyehudhuria mafunzo hayo, Elizabeth Richard, amesema mafunzo hayo yana msaada mkubwa kwo watakapoanza kufundisha shuleni watawasaidia wanafunzi kutatua changamoto zinazowakumba.
Naye Mratibu wa dawati la jinsia Chuo cha Ualimu Butimba, Lilian Nyaga, amesema “Tunafurahi kupata mafunzo haya ambayo yatatusaidia kuboresha utendaji kazi wetu kama taasisi na kuzingatia usawa wa kijinsia,”amesema.