30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

FANIKIO KATIKA MAKUSANYO KODI MBALIMBALI

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM


HIVI karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekutana watumishi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara(TANTRADE) kwaajili ya kuwapa elimu ya kodi mbalimbali.

Huo ni utaratibu ambao TRA imejiwekea ili kuhakikisha elimu ya kodi inaenea kwa wadau mbalimbali wa kodi nchi nzima.

Katika semina hiyo ya siku moja iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi za TANTRADE jijini Dar es Salaam, wafanyakazi hao waliweza kufundishwa mada mbalimbali zinazohusiana na kodi zikiwemo zile za mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2017 pamoja na kodi ya majengo.

Hadi sasa katika kipindi cha miezi sita iliyopita, mamlaka hiyo imeshafanya jumla ya semina 137 kwa wafanyakazi wa serikali, Asasi za Kiraia, wafanyabiashara pamoja na vikundi mbalimbali.

Lengo kuu la semina hizo kwa wadau ni ili kuongeza ufahamu katika masuala ya kodi pamoja na kuongeza uhiyari wa wao kulipa kodi kama ambavyo sheria inavyolekeza.

Afisa Mkuu wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Rose Mahendeka anasema kuwa TRA imejiwekea utaratibu wa kuendesha semina za elimu mbalimbali za kodi ili kuwawezesha kuwa na uelewa lakini pia kuwa mabalozi wazuri kwa wengine ambao mamlaka haijawafikia.

Anasema katika kuhakikisha elimu ya kodi inamfikia kila mdau wa kodi, kupitia maofisa wake nchi nzima TRA imejiwekea utaratibu wa kuwafuata baadhi ya wadau wake katika maeneo yao ya biashara, wengine katika ofisi zao huku wengine wakialikwa katika kumbi ambazo zitakuwa zimeandaliwa.

Anasema kila mwenye kipato anatakiwa kulipa kodi na kwamba kila baada ya kumaliza kupata huduma kutoka kwa mfanyabiashara mteja anatakiwa kudai risiti ili apate uhakika wa kodi aliyolipa imefika sehemu inakostahili.

Anaongeza kuwa, sambamba na mteja kudai risiti pia mfanyabiashara anawajibu wa kutoa risiti kila anapofanya mauzo kwa mujibu wa sheria ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aidha kuhusu kodi ya majengo, anasema kuwa kodi ya majengo huanza kulipwa Julai mosi ya mwaka wa fedha husika hadi Juni 30 ya mwaka unaofuatia.

Anasema kila mmiliki wa jengo au nyumba anatakiwa kulipa kodi hiyo mapema ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima na kwamba kodi hiyo hulipwa kwa mwaka mara moja.

Anasema kodi ya majengo  hulipwa na kila mtu anayemiliki jengo au nyumba hata kama ni mtumishi wa serikali kama ambavyo sheria inavyoelekeza.

Rose anaongeza kuwa huu ni muda muafaka kwa kila mwananchi ambaye atakuwa hajalipia jengo au nyumba yake kodi ya majengo kwenda kulipia badala ya kusubiri siku za mwisho ambazo huwa na changamoto mbalimbali.

Anasema kumekuwa na mafanikio katika makusanyo ya kodi mbalimbali kutokana na uzalendo wa baadhi ya wananchi na kwamba mamlaka hiyo inaendelea kuwasisitizia wengine ambao bado hawajawa na utayari katika kulipa kodi kujitokeza kwa faida ya taifa lao.

Anasema kwa kulipa kodi, serikali itaweza kutekeleza majukumu yake ya kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wake.

Anaongeza kila mwenye kipato anatakiwa kuwa mzalendo katika ulipaji wa kodi ili kuiwezesha serikali kufanikisha malengo yake iliyojiwekea ya kufanya maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles