Bakari Kimwanga, MOROGORO
SERIKALI imekabidhi rasmi eneo la mradi wa umeme wa maporomoko ya Mto Rufiji (RHPP), kwa mkandarasi Kampuni ya Arab Contractors kutoka nchini Misri, huku Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani akitaja manufaa tisa ya mradi huo.
Hatua hiyo sasa inaashiria kuanza kwa kazi ya ujenzi wa mradi huo ambao utazalisha megawati 2,115 ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya taifa na kuifanya Tanzania kuwa na umeme mwingi na wa uhakika.
Akizungumza jana wakati wa kukabidhi mradi huo kwa mkandarasi katika hafla iliyofanyika ndani ya Pori la Akiba la Selous, Dk. Kalemani alisema hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli kusimamia uamuzi wa ujenzi wa mradi huo mkubwa.
Alisema mradi huo ulibuniwa kwa muda tangu mwaka 1970 ambapo kazi ya uchambuzi ilifanyika, lakini haukutekelezwa kwa sababu ya gharama zake kuwa kubwa.
“Wakati ule (1970) mahitaji ya umeme yalikuwa megawati 100. Lakini leo mahitaji ya umeme ni makubwa sana. Na ilipangwa kwa wakati ule kutekelezwa kwa awamu ambapo ungeanza na megawati 400, awamu ya pili 800 na baadaye megawati 900. Hatua tuliyofikia leo ndiko Serikali ya awamu ya tano inataka ya Tanzania ya viwanda.
“Huu ni mradi wa manufaa, miji yote iliyozunguka mradi huu itakua kwa kasi sambamba na uzalishaji wa umeme,” alisema Dk. Kalemani.
Alisema mkandarasi Arab Contractors atafanya kazi ya kujenga bwawa la umeme ikiwamo kingo za kuta pamoja na kujenga vituo vya kuzalisha umeme.
“Ninapenda mtekeleze mradi huu kwa wakati na kwa ufanisi ili kuondoa mashaka kwa watu ambao wenye shaka. Leo mnakabidhiwa eneo la kazi, ni matumaini yetu mtaifanya kazi hii kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na umeme.
“Na kuanzia leo (jana) wakandarasi msiondoke ‘site’ nyumba zipo, miundombinu ipo, iwe jua, mvua jengeni mradi wakati wote na msiondoke hapa,” alisema.
Alisema pia kitajengwa kituo cha kupoza na kukuza umeme cha kV 400 na njia za kusafirisha umeme kwa msongo wa kV 400 kutoka eneo la mradi hadi Chalinze kwenda Dodoma na Dar es Salaam na utakamilika mwaka 2022.
MANUFAA YA MRADI
Dk. Kalemani alitaja manufaa ya mradi huo ikiwamo kuifanya nchi kuwa na umeme wa uhakika na wa kutosha utakaosaidia maendeleo ya uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu ya wananchi.
Mbali na hiyo, alisema pia nchi itakuwa na maji ya uhakika kwa kilimo cha umwagiliaji, hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao na ufugaji katika eneo lililo chini ya eneo la mradi wa maporomoko ya Mto Rufiji.
“Kuboresha shughuli za utalii katika Pori la Akiba la Selous kwa kuwapo mazingira mazuri ya ustawi wa wanyama pori kutokana na uhakika wa maji wakati wote ya bwawa litakalotokana na ujenzi wa mradi.
“Kuongeza mapato ya nchi kutokana na kustawi kwa shughuli za kitalii katika eneo la mradi. Kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda na sekta mbalimbali za uchumi kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika na wa bei nafuu hivyo kupunguza tatizo la ajira.
“Kupunguza athari za mafuriko ya Mto Rufiji kwa wakazi waliopo maeneo ya Rufiji chini hadi delta ya Mto Rufiji na kuongeza pato la taifa na lishe kutokana na mazao ya uvuvi,” alisema Dk. Kalemani.
MAKAMU WA RAIS ARAB
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Kampuni ya Arab Contractors, Wael Hamdy, alisema umuhimu wa mradi huo si kwa Tanzania tu bali ni kwa Afrika.
Alisema kwa niaba ya Serikali ya Misri, watahakikisha wanatekeleza mradi huo.
Hamdy alisema si mara ya kwanza kupingwa kwani hata walipotekeleza ujenzi wa Bwawa la Azuan walipingwa na mataifa mengine, lakini Tanzania kupitia Mwalimu Julius Nyerere aliwaunga mkono Misri.
“Hata kazi ya kupata zabuni ya mradi huu haikuwa nyepesi, lakini tunaamini kwa usimamizi wa Rais Dk. John Magufuli tunaiona Tanzania ikiwa kwenye mwelekeo sahihi.
“Na katika hili linadhihirisha hata mwaka jana nilipofika hapa Tanzania na Rais Abdufatah Al-sis, ninaiona Tanzania leo ikiwa imepiga hatua kubwa, hapa ni kazi tu,” alisema Hamdy.