Na Clara Matimo, Mwanza
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura)Kanda ya Ziwa, imepanga kuyatumia maonesho ya 16 ya biashara Afrika Mashariki yanayoendelea katika uwanja wa Rock City Mall jijini Mwanza kutoa elimu ya maji nishati ya umeme na gasi kwa wananchi.
Akizungumza na MTANZANIA Digita kwenye viwanja hivyo jana, Meneja wa Ewura Kanda ya Ziwa, George Mhina, amesema kutokana na ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta kutoka nchini Uganda unaopita kwenye baadhi ya mikoa ya kanda hiyo ambayo ni Kagera Shinyanga na Geita wafanyabiashara wanapaswa kufahamu fursa zilizopo ili waweze kushiriki na kujiingizia vipato.
Amesema kupitia maonesho hayo wafanyabiashara watakaofika uwanja wa Rock City Mall kwenye banda la Ewura ambao wana nia ya kushiriki katika ujenzi wa bomba hilo la mafuta watapate elimu ya mambo mbalimbali ikiwemo jinsi ya kujisajili, vigezo wanavyotakiwa kuwa navyo na nyaraka wanazopaswa kuzitumia katika usajili.
“Moja ya kazi zetu ni kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma za nishati na maji, kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu inasema ‘tukuze uzalishaji mali kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu’, Ewura tunasema upatikanaji wa huduma za nishati na maji kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu, hivyo uwepo wetu utawasaidia wananchi watakaokuja kutembelea maonesho haya kupata elimu inayohusiana na udhibiti katika sekta za nishati na maji.
“Mfano ikiwa mfanyabiashara anataka kuanzisha kituo cha mafuta atajua ni nini afanye ili aweze kupata leseni kutoka Ewura lakini vilevile kama anataka kuwekeza kwenye masuala ya nishati ya umeme gesi na maji milango iko wazi, nawakaribisha waje kwenye banda letu maswali yao yote yatajibiwa vizuri pia tutawaelekeza mambo wanayopaswa kuyakamilisha,” amesema Mhina.
Mhina amewasihi wananchi kutembelea maonesho hayo bila kusahau kufika katika banda lao ili wapate elimu kuhusu bili za maji pia ikiwa hawaliziki na sekta ambazo ewura inazisimamia watafahamishwa ni wapi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao na utaratibu wa kushughulikia malalamiko ukoje.
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza, Gabriel Kenene, amesema bidhaa tofauti tofauti zitaoneshwa kwenye maonesho hayo ikiwemo za kilimo, mifugo, chakula, vinjwaji, viwandani, tehema, nishati na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.
“Bidhaa ambazo hatuziruhusu kwenye maonesho haya ni madawa ya kulevya, silaha, milipuko, masuala ya dini na siasa, lakini mbali na huduma na biashara mbalimbali pia kuna vivutio vya aina nyingi kama wanyama pori hai wakiwemo simba, fisi, nyoka aina ya chatu, mamba na wengine wengi pamoja na michezo ya watoto, nawaomba sana wananchi wa Mkoa huu na mikoa jirani wafike wajionee,”amesema Kenene.
Kwa mujibu wa Kenene, TCCIA imechukua tahadhari zote za kuwakinga wananchi wote wanaofika kwenye maonesho hayo na ugonjwa wa UVIKO 19 ambazo ni pamoja na uvaaji wa barako pia kunawa maji tiririka na sabuni kwa kila mtu anayeingia kwenye viwanja hivyo, uwepo wa vitakasa mikono katika kila banda pamoja na watu kukaa mbali kwa kuachiana nafasi.