Na FERDNANDA MBAMILA -DAR ES SALAAM
KATIKA jitihada zinazofanywa na Serikali za maendeleo katika kutekeleza mpango mkakati uliopangwa kwa mwaka wa bajeti 2017/18, malengo stahiki ni  kufanikisha ahadi kwa wananchi.
Mbali na mikutano mbalimbali inayofanywa na Serikali ndani na nje ya nchi katika kukuza na kuleta maendeleo  chanya ya kiuchumi nchini, imekuwa chachu kwa viongozi hao kuleta mwanga  kwa jamii kutokana na mwelekeo mzuri wa nchi kimaendeleo.
Baraza la Mawaziri wa Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika  ambao uliundwa kwa lengo la kusimamia na kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu, ulifanya kikao chake nchini hivi karibuni.
Umoja huo umeleta matumaini  makubwa baada ya mazungumzo yaliyofanywa na mawaziri wake hivi karibuni.
Mbali na uwepo wa mikutano ya hapa na pale inayofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushirikiana na mashirika mbalimbali katika kujadili maendeleo katika suala la udhibiti wa fedha.
Kuna umuhimu na jitihada kufanyika kulinda na kuthamini fedha ya nchi kwa kuweka udhibiti na ulinzi na usalama dhidi ya fedha haramu, ambazo zinatengenezwa na kuingizwa nchini  kwa manufaa ya watu fulani wachache.
Hapo awali kulikuwa hakuna chombo maalumu, taasisi au umoja wowote ambao kwa namna moja au nyingine ungeweza kusimamia na kudhibiti fedha haramu kuingia na kutoka nchini.
Kwa sasa kumekuwa na udhibiti na ulinzi wa hali  ya  juu katika mipaka na sehemu mbalimbali ambazo kuna mwingiliano na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa nchi za Mashariki mwa Kusini mwa Afrika wa Kudhibiti Utakasishaji wa Fedha Haramu (The Eastern and Southen Anti Money Laundering Group, ESAAMLG).
Mkutano huo ulifanyika Zanzibar Septemba 8, mwaka huu katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort, mjini Zanzibar, ulikuwa na lengo la kujuzana na kuelezana hali halisi ya mipaka ya nchi wanachama.
Mkutano huo ulitanguliwa na mkutano wa maofisa waandamizi kutoka nchi wanachama wa umoja huo uliofanyika Septemba 2, mwaka huu.
Rekodi zinaonesha kuwa nchi wanachama ni Angola, Botswana, Comoros, Ethiopia, Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia na Afrika Kusini.
Nchi nyingine ni Rwanda, Swaziland, Seychelles, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri ulifunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa niaba ya Dk. Magufuli.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Mawaziri wote wa nchi wanachama  wa Umoja wa ESAAMLG.
Mbali na hayo, mkutano huo ulijadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na hatua madhubuti iliyofikiwa na nchi wanachama katika kuimarisha mfumo wa Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi.
Aidha, mkutano huo walipitisha mikakati mbalimbali ambayo itasaidia nchi wanachama kuimarisha mipaka ya nchi zao.
Katika muundo wa kiutendaji wa Umoja wa ESAAMLG, unajumuisha Baraza la Mawaziri ESAAMLG (Council of Ministers) na sekretarieti ya ESAAMLG.
Baraza la Mawaziri ndicho chombo cha maamuzi cha mwisho katika umoja na hufanya mikutano ya mwaka kati ya mwezi  Agosti  na Septemba.
Katika mkutano uliofanyika mwaka huu, Tanzania ilikabidhiwa uenyeji wa Umoja wa ESAAMLG kwa kipindi cha mwaka mmoja, ambapo Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, alikabidhiwa kijiti cha Urais wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa ESAAMLG (President of Council) naye Onesmo Makombe, ambaye kwa sasa ni Kamishna wa kitengo cha kudhibiti fedha haramu, huyo ndiye aliyekabidhiwa uwenyekiti wa Mikutano ya Maofisa Waandamizi (Chairman of the Task Force Senior  Officials).