Ramadhan Hassan -Dodoma
UTOAJI wa elimu unaofanywa na wasaidizi wa kisheria maeneo ya kanda ya ziwa, kumetajwa ndiyo sababu ya kupungua mauaji ya vikongwe.
Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na mwakilishi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Kasodeko, Marius Isavika wakati wa ufungaji wa mafunzo rejea ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria Tanzania kwa wasaidizi wa kisheria nchini.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la LSF.
Alisema kupitia mradi wa kuimarisha upatikanaji wa haki kisheria, wameweza kutoa elimu maeneo ya kanda ya ziwa kuhusu na madhara ya mauaji kwa vikongwe.
“Moja kati ya jambo ambalo tunajivunia ni kupungua mauaji kanda ya ziwa, sisi tunatoka Simiyu, sababu ni elimu ambayo tumeitoa…sasa hivi hakuna tena mauaji,” alisema.
Alisema changamoto wanayokutana nayo wasaidizi wa kisheria, ni kuwa wachache hivyo kutokuwafikia watu wengi na kwa wakati.
“Kukabiliana na changamoto hii,tumekuja na mobile kliniki ambazo zinatembea maeneo ya vijijini na kuwafikia watu wengi,”alisema.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala alisema mafunzo hayo ya siku tano yalikuwa kwa ajili ya kujadiliana mambo mbalimbali, ikiwemo jinsi ruzuku wanazotoa zinavyowanufaisha wananchi.
“Tumekuwa hapa kuangalia jinsi gani ruzuku tunazotoa zinawasaidia watu wenye matatizo, walengwa wanafikiwa,”alisema.
Alisema kuna maeneo kina mama wanateseka sababu ya kukosa msaada wa kisheria hususan katika masuala ya migogoro ya ardhi na ndoa.