25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

ELIMU: NJIA PEKEE KUWAOKOA WANAFUNZI BARABARANI

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


UNAWEZA kudhani kuwa ni jambo rahisi kwa mwanafunzi kuvuka barabara, lakini kama hawakupatiwa mafunzo wanaweza kujikuta wakipoteza maisha kwa kugongwa na magari.

Watoto wengi wanaosoma mbali na makazi yao, ambako huwalazimu kuvuka barabara ili kufika shuleni au nyumbani, huwa wana kawaida ya kuvuka barabara kwa ‘mafungu’ huku wakiwa wameshikana mikono (kuvuka kwa pamoja). Hii inaonekana kuwa ni njia nzuri ya kuepuka na shida za waendesha vyombo vya usafiri barabarani ambao baadhi yao hawako makini katika kuwaruhusu waenda kwa mguu kuvuka barabara.

Kuna baadhi ya madereva huwa hawajali kabisa hawawajali kabisa watoto wadogo ambao ndiyo kwanza wanajifunza matumizi ya barabara. 
Kila leo tunasikia habari za wanafunzi wakigongwa na magari na kuachwa na ulemavu huku wengine wakipoteza uhai wao.

Mwaka jana Jeshi la Polisi liliwahi kutoa takwimu za wanafunzi wanaogongwa barabarani.

Lilisema kuwa takribani wanafunzi 78 nchini walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani huku 181 walijeruhiwa katika kipindi cha mwaka 2015.
Takwimu hizo zilitolewa na Mnadhimu wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Fortunatus Muslim wakati wa utoaji zawadi kwa washindi wa shindano la uchoraji alama za usalama barabarani.
Muslim anasema kati ya wanafunzi 78 waliofariki, wavulana walikuwa 40 na wasichana 38, huku majeruhi wakiwa 181 ambapo kati yao wavulana walikuwa 81 na wasichana 81.
Anasema; "maeneo hatarishi ambayo yanaongoza kwa kusababisha ajali za barabarani katika Jiji la Dar es Salaam ni Lumumba, Mnazi mmoja, Mikumi, Mtambani, Boko, Bunju na Kongowe."

Mashindano hayo yalilenga kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi juu ya utumiaji wa alama za usalama barabarani.
"Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha usalama barabarani limeendelea kutoa elimu kwa wanafunzi, madereva na jamii kwa ujumla juu ya matumizi sahihi ya barabarani," anasema Muslim.

Hata hivyo, sheria ya usalama barabarani imeonekana kuwa na kasoro hivyo kuwalazimu wadau mbalimbali wakiwamo wa sekta za umma na binafsi kuwa mstari wa mbele katika kupigia kelele juu ya mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani ya Mwaka 1973 ambayo imeonekana inahitaji maboresho ili kuimarisha sekta ya usafiri nchini.

Zipo kasoro nyingi zilizojitokeza katika sheria hiyo, ikiwamo faini ndogo kwa dereva anayefanya kosa hali ambayo imekuwa ikichangia madereva hao kuendelea kila kukicha kusababisha ajali kwa sababu ya unafuu wa adhabu hiyo.

 

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa),Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Baraza la Watumiaji Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA CCC) na nyinginezo zimekuwa zikiiomba Serikali kufanya maboresho ya sheria hiyo.

Ili ajali zipungue ni lazima kuangaliwe viashiria vitano ambavyo vimekuwa vikichochea ajali na madhara yake ambavyo ni mwendo kasi, uzembe wa madereva na abiria, kofia ngumu,  ulevi na kutofunga mkanda (Seat belt).

Pia sheria ya sasa inatamka zuio la mwendo kasi maeneo machache ni lazima kufanyiwe maboresho na kutamka wazi maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu mfano nyumba za ibada, makazi, maeneo ya shule na mbuga, zuio hili litasaidia kupunguza ajali.

Katika sheria hiyo kuhusu ulevi kifungu cha 45 kina zuia unywaji usifike asilimia 0.5 kwa dereva mzoefu na mchanga 0.02 hivyo ni vyema pia ikatamka na aina za madereva.

Pia uvaaji kofia ngumu kifungu cha 39 (11),  kinawataka madereva wote wa vyombo vya magurudumu mawili na matatu kuvaa lakini haitamki wazi umuhimu wa kofia ngumu na kiwango cha ubora wa kofia hiyo.

Sheria hiyo pia ni kandamizi kwa watoto kwa sababu haitamki juu ya vizuizi vya watoto japokuwa watoto ndiyo wanaohitajika umakini pindi wanapokuwa safarini.


Wakati sheria hiyo ikisisitiza uvaaji mkanda sheria kwa abiria wa siti ya mbele haioneshi umuhimu wa abiria wa siti za nyuma kuvaa mkanda huo wakati abiria hao.

"Wananchi siku zote wao ndiyo wavunja sheria utaona dereva anakatiza mbele bila kuchukua tahadhari yoyote hivyo kama hatutafuata sheria hata tukiletewa mpya ni kazi bure,"anasema Tabitha.  
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (Who), zinaonesha watu milioni 20 hadi 50 hufariki kwa ajali duniani kila mwaka.

Hapa nchini zipo shule nyingi za msingi, sekondari na vyuo zimejengwa kandokando ya barabara hali ambayo imekuwa ikichangia ajali za wanafunzi hao pindi wanapovuka barabara. 
SUMATRA CCC imeona haja ya kuelimisha wanafunzi katika shule mbalimbali elimu ya usalama barabarani ili waweze kujitambua na kuwaelimisha wenzao. 
Elimu kwa wanafunzi hao itasaidia kupunguza ajali miongoni mwa wanafunzi na jamii nzima.

Ofisa Habari wa Elimu kwa Umma wa Sumatra CCC, Nicholous Kinyariri anasema, hadi sasa wamefungua vilabu vya wanafunzi katika shule za msingi na sekondari katika mikoa tisa ya Tanzania bara.

Anataja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza, Kagera, Kigoma, Tabora, Mbeya na Mtwara. 
Anazitaja shule katika Mkoa wa Dar es Salaam zilizonufaika na mafunzo hayo ni shule ya msingi  Mibulani, Oysterbay na Msimbazi Wavulana na sekondari ya Benjamin Mkapa, Kibasila na Makongo.

“Tuliona umuhimu wa kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi kwa kufungua klabu katika baadhi ya shule, pia huwa tunawakusanya na kufanya nao makongamano ili waweze kujadiliana kwa undani changamoto wazipatazo pindi wanapokuwa kwenye vyombo vya usafiri,” anasema Kinyariri.

Anasema tangu waanzishe vilabu hivyo mwaka 2014 wameweza kutoa elimu kwa zaidi ya wanafunzi 2300 na watahakikisha wanafunzi hao wanakuwa mabalozi kimkoa na kitaifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu za SUMATRA CCC Mkoa wa Dar es Salaam, Martha Sepeku ambaye pia ni mlezi wa klabu ya Msimbazi Wavulana anasema ipo haja ya kubadili sheria ya mwaka 1973 ili kuwapunguzia kero wazipatazo wanafunzi na abiria wengine wawapo kwenye vyombo vya usafiri. Pia wanafunzi wanapaswa wapewe elimu ya kujua haki zao na wajibu wao wanapotumia usafiri wa umma.

Anasema ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa na mwendo kasi, Uzembe wa dereva, abiria, kondakta na wamiliki, ulevi wa madereva na makondakta, barabara nyembamba, uchakavu wa magari ya masafa marefu, kuchoka kwa madereva na barabara mbovu.

“Serikali ikifanya jitihada kuangalia viashiria hivi ni imani zetu ajali zitapungua hapa nchini kwani zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa pato la taifa na kuacha watoto wengi yatima,” anasema Martha.

Naye Katibu wa Sumatra CCC, Oscar Kikoyo anasema, kwa kutambua umuhimu wa elimu ya usalama barabarani kwa watoto wameandaa mkakati maalumu wa utungaji insha ili kuelimisha zaidi jamii.

Anasema mkakati huo utaanza kwa wanafunzi wawapo likizo katika kipindi cha mwezi Juni hadi Julai ambapo washindi watatu wa kimkoa watazawadiwa zawadi za aina mbalimbali.

Kikoyo anasema washindi hao pia watashindanishwa kitaifa ambapo washindi watatu wa kitaifa watapata zawadi ili kuhamasisha jamii kusoma na kuelewa masuala mbalimbali yahusiyo usalama barabarani.

“Mkakati wetu sisi ni kuona elimu ya usalama barabarani inaifikia jamii nzima na kuwajengea tabia ya kujali usalama wao kila wanaposafiri. Imani yetu ni kwamba wanafunzi hawa watakuwa ni mabalozi wazuri ambao wataelimisha wenzao na jamii” anasema Kikoyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles