WEMA SEPETU ABADILISHIWA HATI YA MASHTAKA

0
880

Na PATRICIA KIMELEMETA


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeanza kusikiliza kesi inayomkabili msanii wa filamu, Wema Sepetu na wafanyakazi wake wawili, huku upande wa mashtaka ukiiomba mahakama hiyo kubadili hati ya mashtaka.

Akiwasilisha hoja hiyo jana mbele ya Hakimu Thomas Simba, Mawakili upande wa jamhuri, Constantine Kakula na Paulina Fungameza, walianza kuwasomea  upya mashtaka washtakiwa hao ambao ni Wema Sepetu na wafanyakazi wake wawili, Angelina Msigwa na Matrida Abas.

Alidai shtaka la kwanza linalowakabili watuhumiwa hao ni pamoja na kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya ambapo mnamo Februari 4, mwaka huu katika maeneo ya Kunduchi Ununio, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kukutwa na msokoto mmoja na vipisi vya dawa za kulevya aina ya bangi yenye gramu 1.08.

Shtaka la pili linamkabili Wema pekee ambaye anadaiwa kutumia dawa za kulevya kati ya Februari 1 hadi 3, mwaka huu katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, mshtakiwa huyo anadaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya bangi.

Washtakiwa hao wanaotetewa na Wakili Peter Kibatala, walikana mashtaka hayo.

Akisoma maelezo ya mshtakiwa wa kwanza ambaye ni msanii Wema, Wakili Kakula alidai msanii huyo ni miongoni mwa watu waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalam  kuwa anajihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya na Februari  3, mwaka huu alijipeleka kituo cha kati cha polisi na kukamatwa.

Alidai Februari 4, mwaka huu polisi walikwenda nyumbani kwake Ununio kwa ajili ya kufanya ukaguzi wakiwa na mshtakiwa huyo, polisi na shahidi huru na kupatikana na vitu vinavyodhaniwa ni dawa za kulevya.

Alidai Februari 6, mwaka huu, dawa hizo zilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na Februari 8 mkemia huyo alitoa uthibitisho kuwa vitu hivyo ni bangi yenye gramu 1.08.

Pia alidai Februari 8 Wema alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kupimwa mkojo ambapo majibu ya uchunguzi yameonyesha alikuwa na bangi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here