23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Elimu bure kuchangiwa

prof joyce ndalichako*Serikali yatangaza kutoa vibali kupitia ma-RC
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SERIKALI imetangaza kuongeza wigo wa utoaji wa vibali vya kuchangia maendeleo ya elimu kwa hiari kwa mamlaka ya wakuu wa mikoa ili kutoa nafasi kwa wadau mbalimbali wenye nia ya kufanya hivyo.
Hatua hiyo imekuja miezi michache baada ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kutoa waraka kuhusu elimu ya msingi na sekondari kutolewa bila kuwapo ada na michango ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli.
Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali iliyotolewa jana Dar es Salaam na kusainiwa na Msemaji wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Rebecca Kwandu, awali vibali hivyo vilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pekee ili kudhibiti michango holela.
Rebecca alisema pamoja na azma ya Serikali ya kutoa elimu msingi bila malipo, lakini bado haizuii wadau mbalimbali wa elimu kuchangia maendeleo yake kwa hiari.
Alisema wadau wakiamua kuchangia kwa nia ya kushughulikia kero yoyoye iliyopo katika shule wanaruhusiwa kufanya hivyo baada ya kupata kibali.
Rebeca alisema katika kutekeleza dhana ya utoaji wa elimu msingi bila malipo, hadi kufikia Januari, mwaka huu Serikali imetoa elimu hiyo kwa jumla ya wanafunzi 9,771,902
“Kati ya wanafunzi hao, 8,301,759 ni wa elimu ya msingi na 1,470,143 ni wa sekondari ambao wanapatiwa elimu msingi bila malipo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
“Serikali inasisitiza kuwa viongozi wanahusika katika kusimamia utekelezaji wake ambapo kwa upande wa wazazi au walezi, kamati na bodi ya shule pamoja na jamii wao nao wana jukumu la kuelewa majukumu yao ipasavyo,” alisema Rebeca katika taarifa yake.
Alisema kutokana na hali hiyo, juhudi za makusudi zinapaswa kufanywa na viongozi na watendaji wa elimu ili kuwezesha jamii kufahamu wajibu wao katika utekelezaji wa elimu msingi bila malipo na hatimaye kufikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Katika kutekeleza wajibu wake, Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia Januari, mwaka huu imeanza kutoa elimu msingi bila malipo imetoa Waraka wa Elimu Namba 6 wa mwaka jana ambao unafafanua na kubainisha majukumu ya Serikali na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa elimu msingi bila malipo,” ilieleza taarifa hiyo.

WARAKA ELIMU MSINGI BILA MALIPO
Desemba 14, mwaka jana Serikali ilitoa waraka wa elimu msingi bila malipo huku wakiainisha majukumu ya wazazi na walezi.
Kutokana na waraka huo, wazazi na walezi walitakiwa kuanzia Januari mwaka huu kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia yakiwamo madaftari na kalamu na chakula pekee kwa wanafunzi wa kutwa na kugharimia matibabu kwa watoto wao.
Pia wanatakiwa kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo; kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na Serikali na kukemea na kutoa taarifa kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimu msingi bila malipo.
Wazazi na wananchi wengine pia wanatakiwa kuendelea kujitolea nguvukazi na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizoko ndani ya jamii.
Katika waraka huo, Serikali ilisema kwamba wizara ina jukumu la kutenga fedha za kugharamia utayarishaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa kulingana na idadi ya wanafunzi; kutenga fedha kwa ajili ya udhibiti ubora wa shule na kutenga fedha za kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimu msingi bila malipo na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi.
BASHE NA ELIMU
Wiki iliyopita Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alikosoa mpango wa utoaji elimu bure unaoendeshwa na Serikali ya chama chake chini ya Rais Magufuli.
Mbali na kukosoa, ameishauri Serikali kurudi nyuma na kujitafakari kabla ya kuendelea kuutekeleza.
Bashe aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Twaweza wenye jina la Mwanga Mpaya, ambayo ililenga kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko kwenye sekta ya elimu, ikiwamo kuanza kwa mpango wa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari.
“As a nation we are in a crisis (kama nchi tuko kwenye wakati mgumu). Si dhambi kukiri tulifanya kosa katika kuutekeleza mfumo huu wa elimu bure na hatujui tunataka kujenga taifa la namna gani kwa sababu tulishafanya makosa awali. Tunapaswa kukaa mezani na kuanza upya,” alisema.
Alisema Serikali inachokitoa kwa wananchi si elimu bure bali wananchi wanachangia kupitia kodi zao wanazotozwa.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii inayosimamia pia sekta ya elimu, alisema kwa sasa Serikali haifahamu inataka kujenga taifa la namna gani kwa kuwa makosa yalishafanyika miaka ya nyuma katika sekta hiyo.
Bashe alisema nchi kwa sasa iko katika matatizo makubwa ya mfumo wa utoaji wa elimu na Serikali haikujipanga vizuri katika kuuanzisha.
“Tanzania isione aibu kurudi nyuma na kuutafakari mfumo wa elimu. Kuna nchi nyingi duniani ziliwahi kufanya hivyo kwa mfano Marekani mwaka 1991,” alisema Bashe.
Alisema elimu bure inayotolewa sasa haiendani na mazingira halisi ya wananchi kwa kuwa shule nyingi bado ziko katika wakati mgumu kwa kukosa madawati na vitabu.
Bashe alisema tangu mwaka 2006, mawaziri waliokuwa wanaongoza sekta ya elimu walikuwa wanakuja na mikakati ambayo haikuwa na lengo la kuikomboa elimu ya taifa wala kuangalia upimaji wa mafanikio.
Alisema sera ya elimu iliyozinduliwa mwaka 2014 haiinui ubora wa elimu nchini, hivyo Serikali inapaswa kurudi mezani na kujipanga upya katika kuitekeleza.
Bashe alisema umasikini nchini hauwezi kuondoka bila kuwekeza katika elimu, na kwamba hata uanzishwaji wa viwanda utashindwa bila wananchi kuwa na elimu ya kuviendesha.

DK. KATABARO
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Elimu, Dk. Joviter Katabaro, alisema nchi kwa sasa iko vitani kielimu.
Alisema Serikali inatakiwa kujipanga vizuri kuhakikisha mfumo wa elimu unamjega mwanafunzi kimazingira.
Mhadhiri huyo alisema mfumo wa elimu ya Tanzania unatengeneza wanafunzi wasiojua kusoma wala kuandika na kwamba haumjengi mwanafunzi aliyemaliza ama darasa la saba, kidato cha nne, cha sita au chuo kikuu kuwa na uwezo wa kujitegemea.

UFAULU USIO NA TIJA
Alisema zamani shule zilikuwa zinafaulisha mwanafunzi mmoja hadi wawili kwa sababu hakukuwa na shule za kutosha za kupokea wanafunzi, lakini kwa sasa kuna shule nyingi za kata, hivyo idadi kubwa ya wanafunzi wanafaulu bila kuwa na uwezo kwa sababu shule ni nyingi.
“Rais Magufuli ameanzisha mpango wa elimu bure kwa nia njema, lakini washauri wake wa elimu hawajafanya utafiti wa kutosha kubaini ni vipengele gani vipewe kipaumbele,” alisema Dk. Katabaro.

SHULE BINAFSI
Alisema kuongezeka kwa shule binafsi nchini kumetengeneza matabaka, akitolea mfano matokeo ya kidato cha nne yaliyotolewa hivi karibuni kwa shule binafsi kuongoza na zile za Serikali kushika mkia.
Dk. Katabaro alisema kutokuwapo kwa bodi ya walimu kunachangia kuwapo kwa ufaulu mbovu wa wanafunzi nchini, akitolea mfano kuwapo kwa bodi za madaktari, wahandisi, wahasibu na wanasheria.

RIPOTI YA TWAWEZA
Ripoti ya Twaweza inaonyesha asilimia 88 ya wananchi waliohojiwa, wanaamini elimu bure itatekelezwa katika muda uliopangwa na asilimia 76 wanaamini sera hiyo itasaidia kuwa na elimu bora zaidi.
Asilimia 15 ya watu wengine walisema elimu bure haitaboresha elimu wakiamini ongezeko la udahili wa wanafunzi, haliendani na rasilimali zilizopo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Twaweza, utafiti huo ulifanywa kati ya Desemba 10, mwaka jana na Januari 2, mwaka huu ambapo watu 1,894 kutoka Tanzania Bara walihojiwa.
Utafiti huo ulibaini kwamba wazazi walikuwa wanaelemewa na michango ya shule. Asilimia 89 ya wazazi walidai walikuwa wakilipa michango mbalimbali, ambapo kati yao asilimia 80 walisema walikuwa wakilipa hadi Sh. 50,000 kwa mwaka, asilimia nane wakilipa zaidi ya Sh 100,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles