23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Polisi yatangaza mapambano

MTZ IJUMAA newfinal.indd

Silaha kutumika kudhibiti wizi bandarini, bodaboda

Na Asifiwe George, Dar es Salaam
JESHI la Polisi nchini, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), limewataka wanaofanya biashara katika bandari bubu za Pwani ya Bahari ya Hindi kuacha mara moja mchezo huo.
Jeshi hilo limesema kwamba, yeyote atakayekaidi agizo hilo atakumbana na mkono wa sheria, huku likitoa ruhusa kwa askari wake ikibidi kutumia silaha za moto kukabiliana na wafanyabiashara hao.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi (Operesheni na Mafunzo), Nsato Marijani, alisema jeshi lake litatumia nuvu na silaha kama njia ya kuwakamata watakaobainika na ukwepaji huo wa kodi.
Alisema hivi sasa wamejipanga na wameanza kuimarisha doria kudhibiti biashara za magendo katika bandari zote ikiwamo ya Dar es Salaam na kwamba, watakaojaribu kuendelea na vitendo hivyo watakumbana na mkono wa sheria.
“Hatuna dhihaka na suala la ukwepaji kodi tutatumia silaha kwa wale watakaojaribu kukimbiza majahazi yao au kujitosa baharini na hiyo itakuwa ni njia pekee ya kuwakamata,” alisema.
Vitendo vya uhalifu
Akizungumzia suala la wahalifu alisema makundi ya kihalifu yapo karibu dunia nzima na kusema kuwa juhudi zimekuwa zikifanywa na Serikali kupambana na uhalifu unaofanywa na watu waovu.
Alisema kazi kubwa ya jeshi hilo ni kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na ulinzi na usalama imara.
“Tutaendelea na mapambano dhidi ya makundi ya uhalifu mwingine ikiwamo ule wa unyangaji wa kutumia silaha, dawa za kulevya, ujangili, biashara haramu ya binadamu na uhalifu mwingine.
“Tumejipanga vizuri na matukio haya machache yasichukuliwe kuwa ni kukithiri kwa uhalifu hivyo tunawasihi wananchi kuwa na utulivu, waendelee na shughuli zao za uzalishaji mali na watoe taarifa katika vyombo vya dola.
“Jeshi la Polisi na vyombo vingine vyote vya ulinzi na usalama tuko imara kukabiliana na makundi ya kihalifu na wahalifu wote wajue kwamba hawana pa kukimbilia,” alisema.
Vita dhidi ya Bodaboda
Kamishna Marijani, alisema jeshi hilo linaendesha operesheni nchini kote dhidi ya waendesha pikipiki wanaovunja sheria.
Alisema jeshi hilo halina msuguano na waendesha bodaboda bali aliwataka kufuata na kutii sheria za nchi hasa zile za usalama barabarani.
Hata hivyo Marijani alionesha kukerwa na baadhi ya vitendo vinavyofanywa na waendesha bodaboda ikiwa ni pamoja na kupita katika taa nyekundu, jambo alilosema ni hatari kwa usalama wao.
“Waendesha bodaboda pia wamekuwa wakibeba abiria zaidi ya mmoja inajulikana kama mshikaki, kitendo hiki ni kibaya, naomba watambue kuwa ni marufuku kubeba abiri zaidi ya mmoja.
Alisema matukio mengi ya kihalifu na unyang’anyi hufanywa na wahalifu kwa kutumia pikipiki. “Bodaboda wasikubali kuchafuliwa jina na ajira zao hivyo wafanye juhudi za kuwafichua wahalifu,” alisema.
Matumizi ya silaha
Alisema imebainika kuwa baadhi ya silaha zinazomilikiwa na raia zinaazimishwa na kutumika katika matukio ya ujambazi wa kutumia silaha na uhalifu wa makundi au katika mapigano kati ya wakulima na wafugaji.
“Kwa mfano hivi karibuni katika mapambano kati ya Wamasai na Wasonjo kuna watu walikodisha silaha za moto na hata kusabisha mauji sasa wajue polisi tumejipanga na suala hili halina nafasi,” alisema.
Alisema bunduki zote ambazo wamiliki wake wamefariki, kuwa wazee sana au wanaosumbuliwa na maradhi kiasi cha kushindwa kudhibiti uhifadhi na matumizi yake zikabidhiwe mara moja kwenye vituo vya polisi vilivyokaribu.
“Tunawataka wale wote wanaofanya hivyo waache mara moja kwani hapatakuwa na muhali dhidi ya wahalifu hao,” alisema.
Dawa za kulevya
Marijani alisema wamepata mafanikio makubwa kwenye vita dhidi ya dawa za kulevya, hivyo amewataka waingizaji na watumiaji wajue kuwa vita inaendelea.
“Sina haja ya kutaja mikakati yote mipya, itoshe kuwaonya wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya kuwa kila zama na kitabu chake, tutafilisi mali zao zinazotokana na biashara haramu ya dawa za kulevya.
“Tutawafuatilia kokote watakapokimbilia, tutawakamata na kuwarudisha nchini kujibu mashtaka dhidi yao na wale waliokimbia makwao na wako hapa tutawakamata na kuwarudisha huko walikotenda uhalifu.
“Tanzania si maficho ya uhalifu, tutawachukulia hatua wote wanaojishughulisha na biashara pamoja na watumiaji wa dawa hizi,” alisema.
Nidhamu
Akizungumzia suala la nidhamu alisema hawana shaka na watendaji wao, wengi wao ni waadilifu na wenye ujuzi mkubwa wa utendaji na moyo wa kizalendo.
“Wachache wanaotuchafua tutawashughulikia bila muhali na kwa hili tunaahidi kulifanya bila woga wala kificho, tunaomba Watanzania watoe taarifa kwa viongozi juu ya mwenendo usio wa maadili miongoni mwetu.
“Sisi ni jeshi na tunawajibika kwenye mamlaka za kiraia na wananchi kwa ujumla wake, hivyo watabaki kuwa jeshi na tutasimamia sheria na hatutakuwa na huruma kwa wahalifu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles