KINSHASA, DRC
SHIRIKA la Afya Duniani limesema kwamba visa 200 vya ugonjwa wa Ebola vimerekodiwa tokea mlipuko huo ulipozuka Agosti mosi, huku wagonjwa 165 wakiwa wamethibitishwa kwa vipimo vya maabara na 35 wakitajwa kuwa wanaweza kuwa na ugonjwa huo.
Wafanyakazi wanaotoa misaada ya kibinadamu, wanajaribu kutuliza hofu katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lililoharibiwa kwa mapigano, ambako watu 125 tayari wameshapoteza maisha huku virusi hivyo vikiwa vinaendelea kusambaa.
Shirika hilo limeeleza wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa idadi hiyo ya maambukizi katika wiki za hivi karibuni, hususan katika mji wa Beni uliopo karibu na mpaka wa Uganda.