26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

DK. NDUGULILE:SERIKALI ITATOA MWONGOZO WA UTOAJI DAWA

Na JOHANES RESPICHIUS, DAR ES SALAAM

SERIKALI imesema kabla ya mwisho wa mwaka huu itatoa mwongozo wa utoaji wa dawa na matibabu katika vituo vya afya na hospitali.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, katika uzinduzi wa cheti cha mfumo wa uhakiki ubora wa huduma za kiwango cha kimataifa cha ISO.

Dk. Ndugulile alisema, Serikali imeamua kufanya hivyo kutokana na mwongozo uliokuwapo tayari umepitwa na wakati hivyo mwongozo huo mpya utahakikisha kila aina ya ugonjwa katika ngazi mbalimbali tunaainishiwa aina ya dawa inayopaswa kutumika.

“Kama nchi na dunia nzima hali ya usugu wa madawa unazidi kukua kwa kiasi kikubwa, hivyo Serikali inatarajia kabla ya mwisho wa mwaka kutoa mwongozo wa utoaji wa dawa na matibabu kwa sababu uliokuwepo umepitwa na wakati.

“Kila aina ya ugonjwa kwa ngazi mbalimbali tutaainisha aina ya dawa ambayo inapaswa kutumika, pia itahakikisha inaimarisha kamati za utoaji wa dawa katika ngazi husika kuhakikisha zinatolewa kwa mujibu wa mwongozo,” alisema Dk. Ndugulile.

Aidha, alisema upatikanaji wa dawa muhimu aina 135 ambazo zinatambuliwa na Serikali umefikia asilimia 80, kwamba wanatarajia kwenye vituo vya afya vya umma upatikanaji wa dawa hizo usipungue asilimi 80.

“Katika hali ya utoaji huduma, moja ya changamoto ambayo imekuwa ikishuhudiwa ni utoaji wa dawa usiozingatia msingi na mara nyingi soko ndilo linasema dawa gani itolewe, hivyo kila mtu kama atakuwa anajiamulia kutoa dawa kwa vile anavyoona inafaa ni hakika kuwa dawa hizi hazitatosha.

“Udhibiti wa ubora wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi umeimarika hasa ukilinganisha na jinsi Rais Dk John Magufuli alivyoongeza nguvu katika sekta ya afya, ambapo bajeti ya dawa imeongezeka sana kutoka Sh bilioni 40 hadi zaidi ya Sh bilioni 200,” alisema Dk. Ndugulile.

Aidha, alisema TFDA kupewa cheti hicho ni hatua kubwa na kwamba imeonesha kwa jinsi gani mamlaka hiyo ilivyoboresha utoaji wa huduma zake hadi kufahamika kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, alisema mamlaka hiyo imekuwa ikitekeleza mfumo wa uhakiki ubora wa huduma kuanzia mwaka 2005 baada ya kufanya tathmini ya namna bora ya kufanya shuguli za udhibiti kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wateja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles