Na Nora Damian, Mtanzania Digital-Dodoma
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango amewataka Watanzania kujivunia miaka 60 ya Muungano na kuuombea uendelee kudumu huku wakizingatia falsafa za 4R yaani maridhiano, ustahamilivu, mageuzi na kujenga upya.
Akizungumza Aprili 22,2024 wakati wa maombi na dua ya kuliombea taifa yaliyofanyika katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, amesema ni baraka kwa taifa kufikia umri huo kwa sababu yako mataifa yaliyojaribu kuungana lakini hayakufanikiwa.
“Mengine yaliungana lakini muungano haukudumu, muungano wetu umekuwa tofauti na kudumu kwa zaidi ya nusu karne. Hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kutufikisha hapa, jukumu letu ni kuendelea kuulinda na kuutetea kwa vitendo,” amesema Dk. Mpango.
Amesema katika kipindi cha miaka 60 taifa limepiga hatua katika mambo mbalimbali kama vile ya huduma za kijamii yaani elimu, afya, maji, barabara, umeme na ustawi wa jamii na kuhakikisha usalama wa wananchi na chakula.
Makamu wa Rais amewataka Watanzania kuwajibika kwa kuendelea kukabiliana na mmonyoko wa maadili ikiwemo uhalifu, ukatili, matumizi ya dawa za kulevya na mengine ambayo hayampendezi Mungu.
“Kuna madai kwamba haki haitendeki, vyombo vya ulinzi na usalama vipo tufuate njia hiyo tutakwenda vizuri. Panapokuwa na madai ya mauaji ya raia au kuteswa tuyapeleke kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na tutayafanyia kazi kwa uadilifu,” amesema Dk. Mpango.
Kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amewahakikishia Watanzania kwamba hawatasita kuchukua hatua pale ambapo watajiridhisha makosa yamefanyika.
“Rais ameshatoa maelekezo wizara zote zinawajibika kutoa maelekezo pale ambapo palikuwa na hoja zilizotolewa na CAG,” amesema.
Dk. Mpango pia ameelekeza mihimili yote ya dola ifanye kazi kwa ushirikiano na kila Mtanzania aitumikie nchi katika nafasi yake kwa haki, uadilifu na uzalendo.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Seleman Jaffo, amesema kazi kubwa imefanyika katika kutatua kero za muungano tangu mwaka 2006 ambapo 22 zimetatuliwa kati ya 25.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema vijana wa sasa wanalo deni kwa Watanzania kuhakikisha wanaulinda na kuutetea muungano uendelee kudumu kwa faida ya vizazi vijavyo.
“Miaka 60 ni mingi, tuna imani tutasimama imara katika miaka 60 mingine, tumefanya mazuri kuhakikisha muungano unaendelea kudumu ili vizazi vinavyokuja waukute,” amesema Abdulla.
Hafla hiyo imehusisha viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali ya Kikristo na Kiislam ambao walifanya maombi na dua na kuwaasa Watanzania kuendelea kuimarisha umoja, mshikamano na uzalendo.