NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI Mtendaji wa Kampuni ya IPP Media, Dk.Reginald Mengi ametoa msaada wa madawati yenye thamani ya Sh milioni 70 kwa wilaya za Bagamoyo, Pwani   na Handeni, Tanga kuiwezesha sekta ya elimu nchini.
Akizungumza   Dar es Salaam jana na wakuu wa wilaya hizo  na viongozi wa halmashauri, Mengi alisema msaada huo utasaidia kuondoa changamoto iliyopo katika sekta ya elimu nchini.
Alisema ana imani ushirikiano wa dhati utasaidia kupatikana kwa wingi  madawati hayo ambayo Rais Dk. John Magufuli aliagiza jamii kuchangia kuondoa tatizo la watoto kukaa chini.
“Anayefahamu matunda ya elimu ni taifa zima ni imani yangu madawati yakipatikana na changamoto zilizopo sasa zikatokomezwa kila mmoja atafaidi huduma za wataalam watakaopatikana kwenye fani mbalimbali,” alisema   Mengi.
Alisema wakati umefika sasa kwa viongozi kutumia fursa walizonazo kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu nchini.
Mengi alisema ushirikiano wa dhati kati ya viongozi na wananchi utasaidia kuleta maendeleo nchini katika sekta mbalimbali.
Pia alisema ni vema viongozi wakaacha uoga wa kutumbuliwa na badala yake wafanyekazi kwa maslahi ya jamii na taifa Kwa ujumla.
Mengi aliwaahidi viongozi hao kushirikiana nao kwa karibu katika kuendesha kampeni za upatikanaji wa madawati.
Alisema fedha hizo alizozitoa zitumike kununua madawati 500 Kwa wilaya hizo mbili na anaamini atakuwa amesaidia kupunguza kero kwa watoto hao.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Husna Msangi alisema wilaya yake inakabiliwa na upungufu wa madawati 752,000.
“Tunashukuru kwa sasa tuna madawati 4,000 hivyo tukipata mengine angalau tutaondoa changamoto iliyopo sasa,” alisema Husna.
Alisema jamii ijitokeze kuiwezesha sekta hiyo ili taifa linufaike na zao la elimu ambalo litatoa wataalam wa fani mbalimbali.